Dunia imekuwa inawahadaa wengi kwamba kipo kitu kimoja ambacho wakikijua na kukifanya basi maisha yao yatakuwa bora, mafanikio kwao itakuwa uhakika. Watu wamekuwa wakidanganyika kwamba kuna kitu wakikifanya mara moja tu basi maisha yao yanabadilika kabisa.

Kwa imani hiyo, watu wamekuwa wanatumia muda mwingi kutafuta kitu hicho ambacho kama wakifanya mara moja maisha yao yanakuwa bora zaidi. Na wamekuwa hawakipati, hivyo wanaishia kuamini kwamba huenda hawana bahati, au kuna watu wanawazuia wasifanikiwe.

siyo ajali

Ukweli ni kwamba, hakuna kitu kimoja pekee ambacho ukifanya utakuwa na uhakika wa mafanikio. Na wala hakuna kitu ambacho ukifanya mara moja basi mafanikio nje nje. Mafanikio ni mchakato badala ya tukio. Mafanikio ni matokeo ya mapambano ya muda mrefu, ya kufanya vitu vingi, ya kurudia rudia kufanya vitu ambavyo kwa mara moja havina matokeo makubwa.

Mafanikio ni mkusanyiko wa hatua ndogo ndogo nyingi sana ambazo mtu anachukua kila siku, kwa muda mrefu.

SOMA; UKURASA WA 1077; Mambo Madogo Yasiyo Na Hatia Yanapoanza Kuzalisha Hatia Kubwa…

Ili kurahisisha safari yako ya mafanikio, kwanza usitafute njia ya mkato, maana njia yoyote ya mkato inaishia kuwa njia ndefu. Pili usihangaike kutafuta kitu kimoja ambacho utafanya mara moja ufanikiwe, badala yake kuwa tayari kufanya kila kitu, kuwa tayari kuchukua kila hatua ili kupata kile unachotaka.

Unachohitaji kila siku ni kuamka na ndoto yako kubwa, kujua wapi unapokwenda, kisha kuangalia kila unachokutana nacho kila siku, kinachangiaje wewe kufikia ndoto kubwa uliyonayo.

Usijiwekee mpaka kwamba mimi huwa sifanyi hivyo, au nasubiri kitu fulani, kila kinachokuja mbele yako ambacho kinaendana na ndoto yako, kiwe kikubwa au kidogo, kiwe rahisi au kigumu, ni wajibu wako kuchukua hatua.

Chukua kila hatua inayokufaa kuchukua kwenye kila hali unayojikuta, huwezi kujua kipi pekee kitakachokufikisha kwenye mafanikio.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog