Rafiki yangu, hongera kwa kufika ukingoni mwa juma hili la 14 kwa mwaka huu 2018. Nikukumbushe kwamba ukiondoa siku, basi kipimo kingine muhimu cha kutumia kuangalia mwenendo wako ni wiki. Kwa siku saba, na masaa 168, ni njia nzuri ya kupanga na kutathmini kila unachofanya.

Na kwa wale ambao wameajiriwa, na wakati huo huo wanafanya vitu vya ziada, njia pekee ya kuweza kuendelea na vyote kwa pamoja ni kutawala wiki yako. Kwa sababu kuna siku utabanwa, lakini kwa siku saba za wiki, hukosi siku ambazo unapata nafasi ya kufanya yale muhimu.

Karibu kwenye 5 ZA JUMA ambapo nimekuwa nakushirikisha mambo matano niliyojifunza na kukutana nayo kwa juma zima, ni mambo ambayo hata wewe rafiki yangu unaweza kujifunza kitu na kuyafanya maisha yako kuwa bora zaidi.

#1 KITABU NILICHOSOMA; MFALME WA AKILI, MWILI NA MATUKIO.

Juma hili la 14 nimefanikiwa kusoma vitabu viwili na cha tatu nikiendelea kukisoma. Na hapa nakushirikisha kitabu kimoja katika nilivyosoma ambacho ni kitabu cha mwandishi James Allen kinachoitwa MAN; KING OF MIND, BODY AND CIRCUMSTANCE.

Najua ukimsikia James Allen unajua kitu kinachohusu Akili na fikra kinahusika hapo. Kwa sababu huyu ni mwandishi wa kitabu maarufu cha AS A MAN THINKETH. Nina kitabu chenye mkusanyiko wa vitabu vyake 19, hivyo ni hazina kubwa nimekuwa naipata kupitia vitabu vyake.

photo_2018-02-18_17-05-44

Kwenye kitabu hichi cha mtu kama mfalme wa akili mwili na matukio, James anaendelea kutusisitiza kuhusu nguvu kubwa ya akili zetu katika kutengeneza mazingira yetu. James anasema japokuwa kuna wakati hatuwezi kubadili yale yanayotokea, bado tuna uwezo wa kubadili tunayafikiriaje.

Kwenye kitabu hichi, kuna sura 7 lakini zipo tatu ambazo nimejifunza mengi zaidi na hapa nitakushirikisha mbili.

Kwenye sura inayohusu MWILI, Allen anasema; magonjwa ambayo watu wengi wanakuwa nayo, yanasababishwa na mawazo ambayo yanatawala akili zao. Mwandishi anasema, mara nyingi watu ndani yao wanakuwa na ubishi unaoendelea, ambapo hawataki kukubali hali fulani inayowatokea kwenye maisha, hivyo wanakaribisha ugonjwa ili uwe sababu. Mwandishi anasema huwezi kukuta wanyama wa mwituni wakiugua magonjwa kama ya binadamu kwa sababu wanyama hao wameyakubali mazingira yao na hawajaribu kushindana au kukataa chochote. Wanyama wanaishi kulingana na mazingira yao na hilo linawafanya kuwa imara, kama sisi binadamu tutaishi kulingana na mazingira na asili zetu, basi tutakuwa imara zaidi.

Kwenye sura ya umasikini mwandishi anasema; umasikini haupo mfukoni, bali upo kwenye akili ya mtu. Kujitoa kufanya kazi kwa juhudi ndiyo njia pekee ya kuondoka kwenye umasikini. Allen anasisitiza; mafanikio, heshima na ushawishi mara zote vinaenda kwa yule ambaye anaweka juhudi kwenye shughuli zake na kuacha kujihusisha na mambo ya wengine. Je wewe unaweka muda wa kutosha kwenye shughuli zako au unajihusisha na mambo ya wengine, ambayo hayakuhusu?

Tumia akili yako vizuri, tawala akili yako kwa fikra chanya, fikra za mafanikio, fikra kwamba unaweza na hicho ndiyo kitakachotokea kwenye maisha yako.

#2 MAKALA YA WIKI; RAFIKI PEKEE AMBAYE HATAKUACHA KWA NAMNA YOYOTE ILE.

Kile ambacho mwandishi James Allen anatufundisha kwenye kazi zake kinafanya kazi mara zote. Wiki hii nimekuwa nafikiria sana kuhusu ufanyaji wa kazi, kwa sababu kuna watu naona hawafanyi kazi, lakini kwa nje wanalalamika kama vile wanafanya kazi mno. Niliandika makala ya rafiki ambaye unapaswa kuambatana naye kabla hata ya kusoma kitabu cha James Allen ambapo nako amesisitiza sana kazi.

Kama hukusoma makala ya wiki, yenye sababu kumi kwa nini unapaswa kupenda mno kazi, na moja ya sababu hizo ni kwamba KUFIA KAZINI NI USHUJAA, basi isome hapa; Ambatana Kwa Umakini Na Rafiki Huyu Mmoja Na Kwa Uhakika Lazima Utafanikiwa (Mambo 10 Ya Kuzingatia Ili Kufanikiwa Kwenye Kazi). (https://amkamtanzania.com/2018/04/06/ambatana-kwa-umakini-na-rafiki-huyu-mmoja-na-kwa-uhakika-lazima-utafanikiwa-mambo-10-ya-kuzingatia-ili-kufanikiwa-kwenye-kazi/)

#2 NYONGEZA; MAKALA NNE NZURI ULIZOKOSA ULIPOKUWA UNAKULA PASAKA.

Mwisho wa wiki iliyopita, ilikuwa mapumziko marefu ya sikukuu ya pasaka, kuanzia ijumaa kuu mpaka jumatatu ya pasaka. Katika siku zote hizo kulikuwa na makala nzuri zinaenda hewani, lakini nimegundua wengi hawakuzipata kwa sababu walikuwa mapumzikoni.

Hapa nimekupa nafasi ya kusoma tena makala hizo nne;

Njia Kumi (10) Za Kuyafanya Maisha Yako Kuwa Rahisi Bila Ya Kuyarahisisha. (https://amkamtanzania.com/2018/03/30/njia-kumi-10-za-kuyafanya-maisha-yako-kuwa-rahisi-bila-ya-kuyarahisisha/)

KITABU CHA APRIL 2018; What winners do to win (wanachofanya washindi kinachowapelekea kushinda). (https://amkamtanzania.com/2018/04/01/kitabu-cha-april-2018-what-winners-do-to-win-wanachofanya-washindi-kinachowapelekea-kushinda/)

USHAURI; Jinsi Ya Kusimamia Miradi Ukiwa Bado Umeajiriwa Na Jinsi Ya Kumshawishi Mwenza Wako Kuielewa Ndoto Yako Ya Mafanikio Makubwa.( https://amkamtanzania.com/2018/04/02/ushauri-jinsi-ya-kusimamia-miradi-ukiwa-bado-umeajiriwa-na-jinsi-ya-kumshawishi-mwenza-wako-kuielewa-ndoto-yako-ya-mafanikio-makubwa/)

#TANO ZA JUMA #13 2018; Saa Ya Kuishi Na Saa Ya Kupenda, Njia Kumi Za Kufanya Maisha Rahisi, Kama Unajua Kila Siku Ya Wiki Hufanyi Kazi Vya Kutosha Na Kipaji Hakina Thamani Yoyote. (https://amkamtanzania.com/2018/04/01/tano-za-juma-13-2018-saa-ya-kuishi-na-saa-ya-kupenda-njia-kumi-za-kufanya-maisha-rahisi-kama-unajua-kila-siku-ya-wiki-hufanyi-kazi-vya-kutosha-na-kipaji-hakina-thamani-yoyote/)

#3 NILICHOJIFUNZA; JINSI YA KUEPUKA KUTUMIWA KUWATAPELI WENGINE.

Juma hili, mke wangu aliibiwa simu yake, sasa baada ya kuwa ameibiwa, tulifunga line zilizokuwa kwenye simu hiyo na kuzifungua upya, tukijua hilo halitakuwa tatizo kubwa, na tukijua hakuna haja ya kupoteza muda kuhangaika kupata simu hiyo, licha ya kwamba taarifa ilitolewa polisi iwapo lolote litatokea.

Sasa kesho yake nilishangaa kupokea ujumbe mfupi, ambao unasomeka kama umetumwa na mke wangu, ila sasa amenitumia mimi, akitaka fedha kwa sababu amekwama na mzigo njiani, muda siyo mrefu tukaanza kupokea simu za ndugu, jamaa na marafiki, wakitaka kujua kuna shida gani.

Sasa kilichotokea ni hichi, ile simu haikuwa na password, hivyo walioiiba waliweza kuingia kwenye simu na kuona kila kitu na kila aina ya mawasiliano. Pia waliweza kupata namba zote zilizokuwa kwenye simu, hivyo walichofanya ni kuandika ujumbe unaoendana na biashara anayofanya mke wangu, wakionesha kwamba amekwama na mzigo njiani na simu yake imeisha chaji, hivyo atumiwe fedha kwenye simu nyingine na akifika atarejesha, namba ya kutuma fedha waliyoweka ni ya hao matapeli.

Ujumbe ule ulikuwa umeandikwa kwa usahihi mkubwa sana, na wengi walishawishika kwamba ni wa kweli, lakini tunashukuru hakuna aliyetuma fedha kabla ya kujihakikishia kama kweli hiyo shida ipo.

Tumekuwa hatua utaratibu wa kuweka password kwenye simu zetu, na haijawahi kutokea shida yoyote mpaka hapa ambapo simu imeibiwa.

Hii imenifanya kutafakari, kwa simu ninazotumia mimi, kwa jinsi zilivyo na taarifa nyingi, ikitokea imepotea au kuibiwa na ikatua kwenye mikono ya mhalifu, litakuwa janga kubwa sana. Hivyo kwa mara ya kwanza nimeanza kuwa na password kwenye simu na pia kuwa na program ambazo iwapo simu itapotea, basi iweze kufuta kila kitu kabla mtu hajatumia taarifa anazokuta kwenye simu vibaya.

Naamini kipo cha kujifunza kwetu wote, kuhakikisha tunalinda sana taarifa zetu la sivyo zinaweza kutumika kutugeuza sisi kuwa matapeli.

#4 HUDUMA NINAZOTOA; KISIMA CHA MAARIFA TU NDIYO UNAHITAJI;

Wapo watu ambao wanapokea emails za masomo ninazotuma karibu kila siku, wakishukuru kwamba masomo haya yanawasaidia sana. lakini pia wanakuwa wanaomba ushauri wa mambo mbalimbali wanayokuwa wanapitia.

Kwa mfano juma hili nimepata ujumbe wa watu siyo chini ya watano wakisema wanafanya kazi sana lakini fedha hawaoni zinaenda wapi, miaka inaenda lakini hawaoni hatua wanazopiga.

Na nimewapa jibu kwamba, wanakosa maarifa sahihi ya fedha. Na wanachopaswa kufanya, ni kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA, ndani ya KISIMA CHA MAARIFA, kuna somo la ELIMU YA MSINGI YA FEDHA, somo muhimu ambalo linakufanya uielewe fedha na isiwe changamoto tena kwako.

Kama na wewe una changamoto zozote ambazo unapitia kwenye maisha, na ungependa sehemu ambapo unaweza kupata maarifa sahihi ya kukusaidia kuzitatua, basi KISIMA CHA MAARIFA ndiyo sehemu pekee unayopaswa kuwa.

Kwa ada ya shilingi elfu 50 kwa mwaka, kila siku utajifunza na kuwa bora zaidi. Tuma ujumbe wenye maneno KISIMA CHA MAARIFA, kwa wasap 0717396253 na nitakupa maelekezo zaidi kuhusu KISIMA CHA MAARIFA.

#5 TAFAKARI YA KUFIKIRISHA; HATA UKISUBIRI UTAPATA.

“Things may come to those who wait … but only the things left by those who hustle.” – Abraham Lincoln

Ukisubiri mpaka kila kitu kiwe vizuri ndiyo uanze, kuna vitu unaweza kupata, lakini jua hili kwa hakika, utakavyopata ni vile vilivyoachwa na wale walioanza kabla hata ya kuwa tayari, wale waliopambana licha ya ugumu.

Kama umeiona fursa ya biashara lakini hujaanza kwa sababu hujawa tayari, utakapokuwa tayari kuanza utapata wateja lakini hao watakuwa ni wateja walioachwa na wale ambao waliweza kuanza kabla hata hawajawa tayari. Chochote unachotaka kwenye maisha yako, usisubiri mpaka uwe tayari kwa kila kitu, bali anza, anza mara moja na utaona hatua zaidi za kupiga.

Nakutakia maandalizi mema ya juma la 15 tunalokwenda kuanza, hakikisha umelipangilia vyema kabla hata ya kulianza.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA www.kisimachamaarifa.co.tz/kujiandikisha

Kupata huduma za Ukocha; www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha

Kujiunga na Kundi la kusoma vitabu; www.amkamtanzania.com/kurasa

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Usomaji