Habari rafiki?
Changamoto ni sehemu ya maisha yetu ya kila siku, hakuna jinsi ambavyo tunaweza kuondokana na changamoto zote kwenye maisha yetu. Kila siku tutakutana na changamoto ambazo pia zitatuingiza kwenye matatizo mbalimbali.
Watu wengi wanapojikuta kwenye matatizo huchukua hatua ambazo zinazidisha tatizo walilonalo, au kukata tamaa na kuachana na tatizo hilo, kitu ambacho kinafanya tatizo lizidi kuwa kubwa.
Na pia watu wengi ambao wamekuwa wakiomba ushauri juu ya changamoto au matatizo wanayopitia, mara nyingi majibu tayari wanakuwa nayo wao wenyewe. Wanachokwenda kupata kwa washauri siyo majibu mapya, bali wanakwenda kuwezeshwa kutumia majibu ambayo tayari wao wenyewe wanayo.
Unaonaje kama na wewe ungeweza kupata nguvu hiyo ya kuweza kutumia majibu yaliyopo ndani yako kutatua changamoto na matatizo yako? Itakuwa bora sana, na hiki ndicho tunakwenda kujadili kwenye makala hii ya leo.
Kuna hatua tano ambazo kama utazifuata, utapata suluhisho bora la tatizo lolote unalopitia kwa sasa au utakalokuja kupitia kwenye maisha yako. kwa kuzijua hatua hizi itakuwa rahisi kwao kuchukua hatua stahiki kwa jambo lolote unalopitia kwenye maisha yako.
Kabla hatujaingia kwenye hatua hizi tano, kuna kitu kimoja muhimu sana unachohitaji kuwa nacho, na kitu hiki ni kijitabu cha kuandika mambo yako muhimu.

http://www.amkamtanzania.com/p/kuwa-tajiri.html

 
Hatua tano za uhakika za kutatua tatizo lolote unalokutana nalo.
Hatua ya kwanza; jua kwa undani tatizo ni nini.
Najua utashangaa lakini ukweli ni kwamba wengi ambao wanakuwa na matatizo huwa hawajui tatizo hasa walilonalo ni nini. Na hivyo wanapokazana kulitatua wanashindwa, kwa sababu kama hujajua kiini cha tatizo huwezi kulitatua.
Mara nyingi watu wamekuwa wakiangalia madhara ya tatizo, badala ya kuangalia chanzo kikuu cha tatizo. Huwezi kutibu tatizo kwa kutibu madhara, badala yake unahitaji kuzama ndani na kujua chanzo hasa cha tatizo ni nini.
Na njia ya uhakika ya kufikia hilo ni kuuliza swali moja muhimu sana, KWA NINI. Uliza swali hili mara tano, yaani uliza kwa hatua tano. Kwa mfano kama tatizo lako ni kipato kidogo kwenye biashara yako, jiulize kwa nini kipato ni kidogo, jibu linaweza kuwa wateja ni wachache, jiulize tena kwa nini wateja ni wachache, hapo utapata majibu mengine, kwa kila jibu jiulize tena kwa nini? Mpaka utafika mahali na kuona hiki ndio kiini kikuu cha tatizo.
Lijue tatizo vizuri, wahenga walisema kulijua tatizo ni nusu ya kulitatua.
SOMA; USHAURI; Hatua Za Kuchukua Pale Unapogundua Umeoa Au Kuolewa Na Mtu Ambaye Tabia Zake Na Zako Haziendani.
Hatua ya pili; orodhesha hatua unazoweza kuchukua.
Baada ya kujua nini hasa ndiyo tatizo, sasa anza kuorodhesha kila hatua unayoweza kuchukua. Andika kila suluhisho linalowezekana kwenye tatizo ulilonalo. Usijihukumu kwamba hiki kinawezekana au hakiwezekani, hiyo siyo hatua hii. Wewe hapa funguka na andika kila aina ya suluhisho unaloweza kufanyia kazi.
Hakikisha unakuwa muwazi na unaandika kila wazo linalokuja kwenye kichwa chako, hata kama litaonekana ni la hovyo au haliwezekani, wewe orodhesha. Ni kwa njia hii ndiyo unaweza kupata njia bora kabisa za kukabiliana na tatizo unalokutana nalo.
Hatua ya tatu; andika faida na hasara za kila suluhisho.
Baada ya kuorodhesha hatua zote unazoweza kuchukua, yaani kila aina ya suluhisho unaloweza kuchukua, sasa unakwenda kuchambua suluhisho moja baada ya jingine.
Andika kila suluhisho na gawa pande mbili, upande mmoja andika faida utakayopata kama utachukua hatua hiyo, na upande wa pili andika hasara za kuchukua hatua hiyo. Andika kila kitu ambacho unafikiria kuhusu suluhisho husika. Na fanya hivi kwa masuluhisho yote uliyoorodhesha kwenye hatua ya pili hapo juu.
Hatua ya nne; chagua suluhisho sahihi.
Baada ya kujua faida na hasara za kila suluhisho, sasa unaweza kuchagua suluhisho sahihi kwako kufanyia kazi. Hapa angalia lile ambalo lina faida kubwa na nzuri na hasara kidogo. Na unapoangalia mambo hayo kuwa makini usifumbwe macho na faida za muda mfupi ambazo mara nyingi zinakuja na hasara za muda mrefu.
Chagua suluhisho ambalo una uhakika unaweza kulifanya na hutokuja kujutia hapo baadaye. Pia hakikisha unaweza kusimamia suluhisho hilo bila ya kutetereka na kuweza kulitetea kwa wengine.
SOMA; Jambo Muhimu Kuzingatia Kabla Ya Kuwasaidia Wengine, Ili Msaada Wako Uwe Bora.
Hatua ya tano; fanya mapitio ya suluhisho ulilochukua.
Ukishachukua hatua siyo mwisho, bali unahitaji kuwa unafanya mapitio na tathmini ya ile hatua uliyochagua kuchukua. Je inaleta matokeo ambayo ulitarajia kupata? Je kuna changamoto nyingine zinaibuka?
Bila ya kufanya tathmini unaweza kushangaa muda unakwenda lakini tatizo linaendelea kuwepo licha ya kupata suluhisho. Unapofanya tathmini unaona ni wapi panahitaji mkazo zaidi na wapi pako vizuri.
Hizo ndizo hatua tano muhimu za kufuata pale unapotaka kutatua tatizo lolote unalokutana nalo. Fuata hatua zote tano kwa mfuatano, usikimbilie hatua ya juu kama ya chini bado hujaikamilisha. Usiwe na haraka, ukishaingia kwenye matatizo unahitaji kutuliza akili yako ndiyo uweze kutatua matatizo hayo.
Kitu kingine muhimu sana kuzingatia ni uvumilivu, usitake kuchukua njia za mkato za kutatua tatizo lolote, maana njia hizi huwa zinaleta matatizo mengine makubwa zaidi.
Fanyia kazi njia hizi tano na kama kuna changamoto zaidi tuwasiliane.
TUPO PAMOJA,
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz