Kwenye jambo lolote lile, mtu anayeanza ni tofauti kabisa na mtu ambaye ameshazoea.

Anayeanza, hasa ambaye anapenda kweli kile anachoanza, anakuwa na hamasa kubwa ya kupiga hatua kubwa.

Anakuwa tayari kujifunza kwa sababu anajua mengi hajui.

Anakuwa tayari kujituma kuliko ilivyo kawaida kwa sababu anaona nafasi za kupiga hatua zaidi.

Ni hatua hizi za mwanzo, kwenye kuanza, zinazowawezesha watu kujijenga kwenye chochote wanachofanya.

Changamoto huwa zinakuja pale watu wanapozoea kile wanachofanya. Wanaanza kufanya kwa mazoea, wanaona hakuna tena kipya cha kujifunza, wanaona wameshajua kila wanachopaswa kujua.

Ni akili hii ya mazoea ndiyo inawafanya watu kupata msongo wa mawazo, kuchoshwa na kile wanachofanya na kuona hakuna kipya kwenye maisha na hata kwenye kila wanachofanya.

SOMA; UKURASA WA 1102; Vitu Vitatu Unavyopaswa Kuvipotezea Ili Kuishi Maisha Yako…

Watu wanapofika hatua hiyo, kipato kinaacha kukua, maisha yanaacha kuwa na hamasa, na watu wanafanya kwa sababu tu inabidi wafanye.

Usikubali kuingia kwenye akili ya mazoea, usikubali kufanya kitu kama ulivyofanya jana na siku zilizopita.

Kila wakati, kuwa na akili ya anayeanza, fanya kitu kama ndiyo unaanza kufanya, fanya kama ndiyo mgeni kabisa.

Kila siku tafuta cha kujifunza kwenye chochote unachofanya, angalia kipya cha kufanya, angalia hatua mpya ya kupiga.

Akili ya anayeanza ndiyo akili bora kwenda nayo maisha yako yote, ndiyo akili ya mafanikio.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog