If thou art a man, admire those who attempt great things, even though they fail – Lucius Annaeus Seneca
Habari za asubuhi ya leo mwanamafanikio?
Tumeipata siku nyingine, siku mpya na ya kipekee kwetu kwenda kuishi kwa msingi wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa TATUA, AMUA NA ONGOZA ambapo tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari WAANGALIE WANAOJARIBU MAKUBWA, HATA KAMA WANASHINDWA…
Kwenye maisha huwa tunazungukwa na watu wa aina mbalimbali,
Huwa tunazungukwa na watu wanaofanya mambo ya kawaida,
Na pia tunazungukwa na watu wanaojaribu kufanya mambo makubwa.
Kwemye jamii ya kawaida, wale wanaofanya mambo ya kawaida ndiyo wanaonekana watu wa kawaida, watu wanaotumia akili.
Lakini wale wanaojaribu mambo makubwa, wanaonekana siyo watu wa kawaida na hawatumii akili.
Lakini mafanikio makubwa huwa yanaenda kwa wale wanaojaribu mambo makubwa, hata kama watashindwa mwanzoni, baadaye wanafanikiwa.
Hivyo kwenye maisha yako, mara zote waangalie wale ambao wanajaribu mambo makubwa, maana hao ndiyo watakaokupa hamasa ya wewe kujaribu makubwa pia.
Hata kama kwa kujaribu hayo makubwa wanashindwa, usikatishwe tamaa na kushindwa kwao kama wanavyokatishwa tamaa wengi, badala yake pata hamasa kwenye udhubutu wao.
Hakuna kazi ngumu kama kuishi kwenye dunia ya kawaida, kuzungukwa na watu wa kawaida, wanaofanya mambo ya kawaida.
Tafuta wale wachache wanaojaribu makubwa, wanaodhubutu kwenda kinyume na kundi kubwa na hao ndiyo watu wa kujifunza kutoka kwao.
Na kama unataka watu wajifunze kutoka kwako, kama unataka watu wahamasike kuchukua hatua kupitia wewe, basi mara zote jaribu mambo makubwa. Usiogope kushindwa, ile nia tu ya kufanya, ni ushindi tosha kwenye maisha yako.
Uwe na siku bora leo, siku ya kujaribu makubwa kwenye maisha yako.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha
Ahsante kocha,hii tafakari imenipa hamasa siku ya leo,kwa sababu naenda kufanya jambo kubwa
LikeLike