Nimewahi kusoma mahali mtu akiandika kwamba kama angeambiwa awaambie watu kitu kimoja wanachopaswa kujifunza kwenye maisha yao ili kufanikiwa, angewaambia wajifunze jinsi ya kuuza.
Kuuza ndiyo kitu muhimu kuliko vyote kwenye maisha na mafanikio, lakini ndiyo kitu kinachodharauliwa na kuogopwa na wengi.

Ukiangalia kwa uhalisia, kila kitu kuhusu maisha ni kuuza. Wafanyabiashara wanauza bidhaa au huduma zao, waajiriwa wanauza muda na utaalamu wao, viongozi wanauza sera zao.
Hata kwenye maisha ya kila siku, maisha yasiyohusisha kazi au biashara, makubaliano yoyote tunayoingia na wengine ni matokeo ya kuuza. Ili kuweza kumshawishi mtu akubaliane na wewe, lazima umuuzie maelezo na ushawishi wako. Lazima umpe sababu za yeye kukubali kitu ambacho hakuwa akikifikiria.
SOMA; UKURASA WA 1103; Tatizo Lako Halihitaji Kutumia Chochote…
Hivyo rafiki, kwa mafanikio yetu, kitu kimoja tunachopaswa kuwa vizuri sana ni kuuza. Lazima uwe vizuri kwenye kuuza, chochote kile ambacho unataka kuipa dunia ili uweze kufanikiwa.
Dunia tunayoishi sasa, kuuza kumekuwa changamoto kwa sababu ya kelele, wapo watu wengi wanaowapigia kelele wale unaowalenga hivyo usipokuwa na mkakati mzuri, kelele zinakupoteza.
Njia ambayo wengi wamekuwa wanatumia ni kupiga kelele zaidi, lakini imekuwa haisaidii.
Jua wale unaowalenga kwa kile unachofanya, jua maumivu wanayopitia, kisha njoo na suluhisho la maumivu yao, wape sababu ya kuamini kwa nini wewe ndiye unayewafaa katika kuondoa maumivu yao.
Kila wakati uza, na jifunze jinsi ya kuwa muuzaji mzuri zaidi. Hilo litakusaidia kuwafikia wengi na kufanikiwa kwenye maisha yako.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog