Moja ya vitu vinavyowazuia watu kufanikiwa, ni kutokujulikana wamesimama upande upi kwenye kila jambo wanalojihusisha nalo kwenye maisha. Wengi huwa wanaonekana kukaa kati kati, wasijulikane kama ni moto au baridi, nyeusi au nyeupe.
Wengi hufikiri kwa kutokuwa na upande, basi hawatamkasirisha yeyote, hawatakosolewa na yeyote na hivyo maisha yao hayatakuwa na changamoto.

Ni kweli kwa kutokuwa na upande, kwa kutokujulikana umesimama wapi kutakuepusha na changamoto nyingi, hutawakasirisha watu na wala hutaibua watu wa kukukosoa, lakini pia hutaweza kufanikiwa.
Upo usemi maarufu kwamba kama kila mtu anakubaliana na wewe, basi kuna kosa kubwa unafanya, na kama hakuna anayekukosoa, basi hakuna kikubwa unachofanya.
Kwenye haya maisha, ni lazima ujulikane umesimama upande upi, lazima watu wajue wanaweza kukutegemea kwa lipi, la sivyo hakuna atakayekutegemea na hutaweza kufanikiwa.
SOMA; Search UKURASA WA 263; Kama Sio Ngumu Ni Laini.
Mafanikio kwenye maisha ni matokeo ya kutegemewa, matokeo ya kuaminiwa, matokeo ya watu kuwa na uhakika kwamba wewe utafanya kile umesema utafanya.
Sasa kama upo katikati, kama hujulikani unasimama wapi, kama hakuna uhakika utafanya au la, inakuwa vigumu watu kukutegemea na kukuamini.
Hata kama unakosea, ni vyema ukajulikana umesimama wapi, angalau watu watajua kipi unaweza kuwafanyia kwa upande huo huo uliokosea.
Hata vitabu vya dini vinasema, ni heri kuwa moto au kuwa baridi, kuliko kuwa vuguvugu. Vuguvugu haijawahi kuwapa watu imani. Bora kuwa moto uambatane na walio moto, au kuwa baridi uambatane na walio baridi, kuliko kuwa vuguvugu ambapo moto wanakukataa, baridi wanakukataa na vuguvugu wenzako wamevurugwa kama wewe.
Julikana unasimamia nini, julikana unafia nini, na hicho ndiyo kitakachokuletea mafanikio yako.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog
Ujumbe bora kabisa, kweli kabisa ndivyo maandiko matakatifu yasamavyo.
Rejea: Basi, kwa sababu una uvuguvugu, wala hu baridi wala moto, nitakutapika utoke katika kinywa changu. Ufunuo wa Yohana 3:16.
LikeLike
Asante sana Samson.
LikeLike