Ushindani ni mkali sana zama hizi, chochote unachofanya, wapo wengine ambao wanakifanya pia. Na hata ukiamua kuwa mbunifu na ukaanzisha kitu chako mwenyewe, watu wakishaona kinafanya kazi watakuiga, huna njia ya kujimilikisha chochote unachofanya, hata kama umekibuni mwenyewe.
Hivyo ili kuepuka ushindani na wale ambao wanafanya kile unachofanya, vipo vitu viwili muhimu sana vya kuzingatia, usipuuze vitu hivi kama kweli unataka kuonekana wa tofauti katikati ya kundi la wengi.

Moja; usiishiwe mawazo mapya.
Mara nyingi utawakuwa watu wanafanya kitu kwa mazoea, wakisema hawana njia nyingine mbadala ya kufanya, au hawana mawazo wanawezaje kufanya kwa utofauti. Hawa ni watu ambao wamekubali kuishiwa mawazo mapya.
Usikubali kabisa kuishiwa mawazo mapya, kwa chochote unachofanya, kila siku fikiria na pata mawazo mapya, njia mpya za kufanya, njia mpya za kuboresha zaidi. Kila wakati jifunze njia mpya unazoweza kutumia kufanya na kuboresha zaidi kile unachofanya.
Siyo lazima kila wazo jipya unalokuwa nalo ulitumie, bali katika mawazo mengi unayopata, jaribu machache na yale yanayoleta matokeo mazuri yatekeleze kwa hatua kubwa. Kwa kufanya hivi watu wataona kila wakati unakuja na vitu vipya na kuwaacha mbali wale wanaofanya kile unachofanya wewe.
SOMA; UKURASA WA 838; Mmoja Kati Ya Wengi Na Mmoja Kati Ya Wachache…
Mbili; endelea kuboresha kile ambacho tayari unafanya.
Mazoea ni mabaya, mazoea yanaua na mazoea yanakaribisha ushindani mkubwa. Kama unafanya leo kama ulivyofanya jana, leo hakuna unachofanya. ukifanya kitu kile kile kila wakati, hata washindani wako wataona udhaifu wako vizuri na kuutumia kwa manufaa yao.
Chochote unachofanya, kila wakati kiboreshe zaidi, kila siku jiulize kipi unaweza kuongeza kwenye kile unachofanya ili watu wakapata thamani zaidi. Na kama ukiangalia, utaona njia nyingi za kuboresha kile unachofanya.
Maamuzi ya kuendelea kuwa juu na tofauti na wengine, au kupotezwa katikati ya wengine yapo ndani yako. Ni juhudi unazoweka kwenye kuifunza na kujaribu mambo mapya ndiyo zitakuweka mbele zaidi ya wengine. Tumia kila nafasi unayoipata kitoa kitu cha ziada na cha tofauti kabisa.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog