Hatua ngumu kwenye maisha na mafanikio ni kufanya maamuzi. Kwa sababu unapofanya maamuzi, maana yake unakubali kuachana na mengine yote na kufanya kile ulichochagua kufanya au kufuata.
Watu wengi hukwepa kufanya maamuzi kwa sababu wanaona kuacha mengine ni hatari kubwa. Kwa mfano kuingia kwenye biashara fulani ni maamuzi magumu kufanya kwa sababu fedha unayoweka kwenye biashara hiyo huwezi kuitumia kwa kitu kingine chochote. Bila ya kusahau kwamba, kuna hatari ya kupoteza fedha hiyo pia.

Hivyo kukosa vingine na hatari ya kupoteza ni vitu vinavyowazuia wengi kufanya maamuzi. Lakini sasa, huwezi kufanikiwa bila ya kufanya maamuzi, hutaweza kupiga hatua yoyote bila ya kujiweka kwenye hatari fulani.
Na hapa ndipo unahitaji kufanya maamuzi ya hekima.
SOMA; UKURASA WA 608; Hasara Ya Kutokufanya Maamuzi Ya Maisha Yako…
Maamuzi ya hekima ni pale unapofanya maamuzi ukijua kwamba kama yatafanikiwa basi utaweza kupiga hatua na kama yatashindwa basi utakuwa umejifunza na kuwa na busara na hekima zaidi.
Iwe utapata au utakosa unachotaka, bado matokeo ni faida kwako. Kwa sababu utakachojifunza kitakusaidia zaidi baadaye.
Hivyo unapojikuta njia panda, unapojikuta na hofu ya kufanya maamuzi kwa sababu hujui matokeo, kumbuka kufanya maamuzi ya hekima. Angalia kila unachoweza kujifunza iwapo utashindwa, kisha fanya maamuzi yako na yasimamie.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog