Ukiacha shamba lenye rutuba bila ya kulifanyia chochote, magugu yataota na kustawi vizuri sana. Lakini magugu siyo kitu unachotaka kwenye shamba lako, ila yamejiotea yenyewe. Ukitaka kusafisha shamba hilo, utahitaji kuweka kazi, tena siyo ndogo.
Hutakuta shamba lenye magugu limejisafisha lenyewe, lakini shamba safi utalikuta lina magugu lenyewe.
Kwa asili, matatizo yanaonekana kama kuja yenyewe, lakini ili kutatua matatizo hayo, tunahitaji kuweka kazi kubwa. Inahitaji nguvu na muda wetu kufanya mambo yaende sawa, hasa baada ya kuwa yamekwenda sivyo.

Kwa kujua hili, ni vyema kuzuia matatizo kabla hayajatokea, kwa kuwa tunajua kwamba, matatizo yatatokea yenyewe, kuzuia ile mianya inayokaribisha matatizo kutaokoa muda na nguvu tunazohitaji kutatua matatizo hayo.
SOMA; UKURASA WA 992; Mambo Yangeweza Kuwa Mabaya Zaidi…
Kila kitu kikiachwa kilivyo, kinaharibika na kuingia kwenye matatizo. Chuma kikiachwa kilivyo kinashika kutu, nyumba ikiachwa ilivyo inapasuka ufa, mahusiano yakiachwa yalivyo yanadorora na kufa, biashara ikiachwa ilivyo inadorora na kufa, kazi ikiachwa ilivyo inachosha na kudumaza.
Kila kitu tunachojihusisha nacho kwenye maisha yetu, jukumu letu la kwanza ni kuhakikisha hatukiachi kilivyo kiasi cha kukaribisha matatizo. Tunahitaji kuchukua hatua kila mara ili kuhakikisha matatizo hayakaribii kwenye kitu hicho.
Kwa sababu nguvu na muda unaoweka kuzuia matatizo ni mdogo kuliko nguvu na muda unaohitaji kutatua matatizo yakishakaribia. Ni rahisi kujenga mahusiano wakati bado yapo vizuri, kuliko kuanza kuyajenga upya yakiwa yameshavunjika. Ni rahisi kuzuia chuma kisipate kutu, kuliko kuondoa kutu ambayo imeshajitengeneza kwenye kutu.
Usiache mambo kama yalivyo, yatakaribisha matatizo ambayo yatakuchukulia muda na nguvu zako nyingi.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog