Hadithi ya Daudi na Goliath ni hadithi ambayo kwa namna tofauti imefundishwa kwenye kila jamii, kuhusu mtu mdogo anayepindua mtu mkubwa na kuleta mabadiliko.
Kila mmoja wetu ni Daudi kwenye eneo fulani, na kuna Goliath ambaye anamsumbua, ambaye ni mkubwa na anatumia ukubwa wake kuwakandamiza wengine.
Iwe ni kwenye kazi, biashara na hata maisha ya kawaida, hakujawahi kuwepo na usawa. Hivyo mara nyingi utaanzia upande wa chini, upande wa Daudi, huku akiwepo Goliath ambaye anaweza kukuharibia kila unachofanya.

Njia bora ya kumshinda Goliath unayemkabili siyo kupigana naye moja kwa moja, bali kukazana kuwa bora kwenye maeneo ambayo Goliath hawezi kuwa bora, kutokana na ukubwa wake.
Kwa mfano kama unaanza biashara ambapo kuna washindani wakubwa, ambao tayari wana uzoefu na wana jina kubwa, kushindana nao moja kwa moja kutawafanya wakuondoe kabisa kwenye biashara hiyo.
Hivyo njia bora ya kuwashinda, au kuwaepuka wasikuumize, ni kuangalia maeneo ya biashara ambayo biashara hiyo haiwezi kufanya vizuri. Kwa mfano biashara nyingi kadiri zinavyozidi kuwa kubwa, ndivyo huduma kwa wateja zinavyozidi kuwa mbovu.
SOMA; UKURASA WA 937; Usishindane Na Mtu Huyu…
Hiyo ina maana kwamba kama utaweka juhudi nyingi kwenye kutoa huduma bora kabisa kwa wateja wako, basi utakuwa na kitu cha kukutofautisha na biashara kubwa, ambazo hazitakuwa na njia ya kukuzidi kwenye hilo.
Lakini ukijidanganya na kutumia njia za kawaida kama kupunguza bei, utakuwa umekaribisha kifo chako mwenyewe. Kwa sababu biashara kubwa zinaweza kupunguza bei maradufu na zisipate hasara kubwa.
Angalia kile ambacho Goliath unayemkabili hawezi kukifanya, kisha kifanye kwa ubora wa hali ya juu sana. Hilo litakutofautisha na wengine wote.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog