Umewahi kujiambia kwamba watu hawaeleweki? Kwamba ulitegemea wafanye kitu fulani halafu wao wakafanya kitu kingine tofauti kabisa?
Ukweli ni kwamba siyo watu hawaeleweki, ila wewe ndiyo huelewi jinsi ya kuwaelewa watu.
Kosa kubwa tunalofanya kwenye kuwaelewa wengine ni kujitumia sisi wenyewe kama kipimo cha kuwaelewa wengine. Kwamba kwa sababu sisi tunafikiria kitu fulani, basi wengine nao wakifikirie pia. Kwamba kwa sababu kitu fulani kwetu ni kizuri au ndiyo sahihi, basi dunia nzima inapaswa kuchukulia kitu hicho kama tunavyochukulia sisi.

Hapo ndipo tunapofanya kosa kubwa na tunaishia kutokuwaelewa wengine.
Njia pekee ya kuwaelewa wengine ni kujua kwamba watu tunatofautiana. Kujua na kukubali kwamba unachoona wewe ni kizuri siyo wote wataona ni kizuri, kile unachofikiria wewe ndiyo sahihi siyo kila mtu ataona ni sahihi. Na hata unachoona siyo sahihi, wapo watakaoona ni sahihi na kufanya.
SOMA; UKURASA WA 1021; Watu Watakaa Upande Wanaotaka Kukaa…
Elewa kwamba watu tunatofautiana, kulingana na imani ambazo tumejengewa, mazingira yaliyotuzunguka na hata kile kinachotusukuma kuchukua hatua tunazochukua.
Ukitaka kumwelewa mtu hata kwa kiasi tu, basi acha kujitumia wewe kama kigezo cha kuwaelewa wengine, na muhimu zaidi, jua watu wanatofautiana na dhana ya nzuri na mbaya, na sahihi au siyo sahihi ina tafsiri tofauti kwa kila mtu.
Utawaelewa wengine kwa kuelewa kwamba siyo kila mtu anafikiria na kuiona dunia kama unavyoiona wewe. Na hilo halimaanishi kwamba wewe ndiyo upo sahihi na wengine wanakosea. Mnaweza kuwa sahihi wote au mnaweza kuwa mnakosea wote.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog