Watu ni changamoto kubwa kwenye mafanikio yako,

Utahitaji watu wa kukusaidia kama wafanyakazi, lakini wengi watakusumbua.

Utahitaji watu wa kushirikiana nao kwenye yale unayofanya,

Lakini wengi watakuangusha.

Utahitaji watu wawe wateja wa kile unachofanya au kuuza,

Lakini wengi hawatakuja kama unavyotaka waje.

Utafika hatua na kupoteza imani na watu, na kuona watu wote ni wale wale, na hakuna ambao wanakufaa wewe.

Mtu Pekee

Lakini napenda nikukumbushe kwamba dunia ina watu zaidi ya bilioni saba kwa kipindi hichi ninachoandika. Hivyo usikusanye kundi la watu bilioni saba na kuwapa tabia moja wakati umekutana na watu wasiozidi 100 kwenye maisha yako.

Hivyo watu ni wengi, wengi mno, na hawawezi kufanana tabia wote.

Lakini je utawezaje kuchagua watu sahihi wa kujihusisha nao? Je utawezaje kupata watu watakaoweza kuendana na wewe, na wasiwe tatizo au mzigo kwako?

Kurahisisha zoezi hili, angalia vitu vitatu, nasema angalia na siyo sikiliza, na vitu hivi viangalie kwenye maisha ya watu hao, na usisikilize chochote ambacho mtu anasema.

Angalia uaminifu, kama mtu siyo mwaminifu kwenye eneo lolote la maisha yake, kaa naye mbali, atakuwa na matatizo makubwa kwako. Kama mtu anadanganya kwa lolote, hata kama ni dogo, jua kuna siku atakudanganya kwenye makubwa na atakuumiza. Kama mtu hajaweza kutimiza makubaliano yake na wengine, hata kama ni madogo kiasi gani, jua atakuletea matatizo makubwa zaidi. Angalia sana uaminifu, asiyekuwa nao, atakuwa tatizo kwako.

Angalia nidhamu ya mtu. Kama mtu hana nidhamu, tegemea matatizo kutoka kwake. Kama mtu hawezi kufanya alichosema au kupanga anafanya, kama mtu hawezi kuwahi mahali anapopaswa kuwahi, kama mtu hawezi kutumia muda na fedha zake vizuri, unafikiri atawezaje kutumia muda na fedha zako vizuri. Nidhamu ni hitaji muhimu, na unahitaji kuliangalia, hasa kwa mambo madogo madogo.

Angalia utayari wa kujifunza wa mtu. Kila mtu kuna kitu ambacho hajui, na kila mtu ana nafasi ya kuwa bora zaidi kwenye chochote anachojua au kufanya. Kama mtu hajui, lakini anajua kwamba anajua, ni mtu hatari. Kama mtu anaona tayari anajua kila kitu, na hana tena cha kujifunza, ni moto wa kukaa nao mbali sana. Angalia utayari wa mtu kujifunza, na kujifunza kwa kila mtu na kwa kila jambo. Angalia unyenyekevu wa mtu katika kupokea yale anayoelekezwa au kufundishwa. Hii itakusaidia kupata mtu sahihi, ambaye anajifunza na kuwa bora zaidi.

SOMA; UKURASA WA 1087; Kigeugeu Cha Watu Inapokuja Kwenye Mafanikio Yako…

Tumia mambo hayo matatu kuwachuja watu wa kujihusisha nao, tumia vigezo hivyo kama mchujo. Kuna vingine muhimu kulingana na unachotaka wewe, lakini kama hivyo vitatu havipo, hivyo vingine vikiwepo vitakuwa chanzo cha matatizo zaidi kwako.

Kwa mfano kama unaangalia mtu msomi, mwenye juhudi na akili nyingi, kama mtu huyo siyo mwaminifu, atatumia juhudi na akili hizo kukumaliza kabisa.

Huwezi kuwakwepa watu, unawahitaji zaidi na zaidi kwenye maisha yako, kitu pekee unachoweza kufanya ni kuchagua vizuri wale unaojihusisha nao, na kila wakati kuwa unafanya mchujo ili kuhakikisha mara zote una watu sahihi.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog