Tofauti kubwa ya wale waliofanikiwa sana na wale ambao hawajafanikiwa ni kwenye fikra zao kuhusu kupata vile vitu wanavyotaka.

Waliofanikiwa sana wanajua wanaweza kupata vyote, vile wanavyovitaka wanaweza kuvipata na hawajiwekei ukomo. Na hata kama hawapati mwanzoni, hawajiumizi kwa sababu hawajapata, bali wanaangalia wanawezaje kupata vyote, na hapo wanapata njia ya kuvipata.

Kwa wale ambao hawajafanikiwa, huwa wanafikiri kwa ukomo, kwamba nikipata hichi basi siwezi kupata kile. Wanaona kupata kila wanachotaka ni kitu kisichowezekana, kwamba kupata kimoja ni kizuizi kupata kingine.

Haki Yako

Mfano mzuri ni kwenye fedha na furaha. Wasiofanikiwa wanafikiria kwamba wakipata fedha hawawezi kupata furaha kama vile fedha zinazuia furaha. Lakini waliofanikiwa sana wanajua wanaweza kupata fedha nyingi na wakawa na furaha pia. Kwa sababu wanajua hakuna ukinzani kati ya fedha na furaha, na wanajua furaha haihusiani sana na fedha.

Kila wakati unapojiambia kwamba huwezi kupata kitu fulani kwa sababu umepata kingine, jiulize je ni kweli au unajiwekea ukomo kwenye kufikiri kwako?

Kila unapofikiria kwamba huwezi kuwa na maisha bora ya kifamilia kwa sababu kazi zako zinakuhitaji kwa muda mrefu sana, jiulize je ni kweli au hutaki tu kufikiria kwa usahihi? Kwa sababu haijalishi kazi zako zinakuhitaji kwa muda mrefu kiasi gani, bado unaweza kupata muda wa kuwa na familia yako. Na vipi umeshafikiria kufanya baadhi ya kazi zako na watu wa familia yako? Au kufanyia kazi nyingine nyumbani? Au kutenga muda mfupi, lakini ambao utakuwa na familia tu na hakuna usumbufu mwingine wowote?

SOMA; UKURASA WA 1252; Matajiri Wa Kweli Hawafilisiki….

Linapokuja swala la mafanikio, unaweza na unapaswa kupata kila kitu. Kama unaelekea kwenye mafanikio na kuna kitu unaona huwezi kupata kwa sababu umepata kingine, kaa chini na utafakari upya, utaona njia ya kupata kila unachotaka.

Ni kweli mafanikio yanahitaji kutoa kafara, lakini kafara tunazotoa ni yale mambo ambayo siyo muhimu. Lakini yale mambo muhimu sana kwetu, mfano furaha, ukuaji wa kiroho, afya, familia na utu wetu binafsi, tunapaswa kuwa navyo kwa wingi zaidi kadiri tunavyofanikiwa. Na hilo linawezekana vizuri sana.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog