Kuna wakati mtu unakwama kwenye kile ambacho unakuwa umepanga kufanya, unakuwa umefika kwenye hali ambayo unaona huwezi kupiga hatua tena.
Na hili linaweza kuwa halisi au inawezekana unalitengeneza.
Linakuwa halisi pale unapokuwa umechukua hatua na kukutana na changamoto ambayo inakuzuia kuendelea kama ulivyotaka kuendelea.

Na inakuwa siyo halisi, yaani unakuwa umetengeneza mkwamo pale unapoona bado hujawa tayari, pale unapojipanga zaidi, pale unapoona mambo yakiwa sawa basi utaanza kufanya. Hapa unakuwa umetengeneza mkwamo kwa sababu hakuna siku utajisikia upo tayari, hakuna siku utaona kila kitu kipo sawa.
SOMA; UKURASA WA 150; Sababu Moja Inayokufanya Unakwama.
Sasa, yote kwa yote, iwe mkwamo ni halisi au ni wa kutengeneza, unapaswa kukumbuka hichi muhimu sana, mkwamo wako hautamsaidia yeyote, siyo wewe wala wale unaojaribu kuwaambia kwamba umekwama.
Njia pekee ambayo mtu anaweza kunufaika, ni wewe kuchukua hatua, kuanza kuondoka kwenye ule mkwamo ambao upo. Kuona kipi unaweza kufanya na kuchukua hatua. Hata kama umekutana na changamoto kubwa, unaangalia kipi cha kufanya na unaanza kufanya. Na kama unajiona hujawa tayari, basi unaanza hivyo hivyo, ukijua kwamba utayari utaendelea kujitengeneza.
Tambua pale unapokuwa umekwama na chukua hatua kuondoka kwenye mkwamo wako. Kuendelea kukaa kwenye mkwamo hakutamsaidia yeyote.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,