Niambie katika hali kama hizi umekuwa unachukua hatua gani;

Umeamka asubuhi na mapema, na huna ulichopanga kufanya kwa muda huo.

Umeenda eneo ulilotakiwa kuwepo, labda kwenye mkutano au darasa, lakini tukio lililopaswa kuanza linachelewa kuanza tofauti na ilivyopanga, hivyo unakuwa na muda ambao huna cha kufanya.

Unasafiri kwenda mahali na huna cha kufanya wakati huo wa safari.

Umekutana na mtu ambaye hamjakutana muda mrefu, baada ya maongezi ya awali, mambo ya kuongelea yanaisha na kila mtu anakuwa hana kipya cha kuongea.

Hizi ni nafasi ambazo tunakutana nazo mara kwa mara, nafasi ambazo tuna muda mfupi ambao hatuna kitu tulichopanga kufanya.

Muda tulionao

Hizi ni nafasi nzuri sana kwa kuwa na utulivu, nafasi nzuri ya kusubiri na kupunguza mwendo wa maisha, nafasi nzuri ya kutafakari maisha.

Lakini tumekuwa hatutumii hivyo muda wetu, badala yake tunakimbilia kwenye usumbufu. Tunapopata nafasi ya kutulia na kutafakari, tunakimbilia kwenye usumbufu, tunakimbilia kufungua simu zetu, tunakimbilia kuingia kwenye mitandao.

SOMA; UKURASA WA 334; Kama Kila Kitu Kitashindikana….

Haya yote ni kulewa kelele, kuepuka kufanya yaliyo muhimu na kutaka uone kuna cha msingi umefanya, wakati ulikuwa umejivuruga na kelele. Watu wengi wanaogopa muda wa utulivu, wanaogopa ukimya hivyo unapojitokeza wanatafuta kila njia ya kukimbia utulivu huo.

Unapopata nafasi ya utulivu, nafasi ya ukimya, usikimbilie kwenye usumbufu, badala yake tulia, sikiliza na tafakari. Huu ndiyo wakati pekee unaoweza kuyatafakari maisha yako na kuweza kuchukua hatua sahihi za kuwa bora zaidi.

Ondoka kwenye ulevi wa kelele na anza kupenda utulivu na ukimya.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha