Kwa dunia tunayoishi sasa, dunia yenye kelele za kila aina, kusikika imekua ni kitu kigumu sana.
Hii ni kwa sababu sasa hivi kila mtu ana jukwaa la kusema, na wale ambao unataka wasikie unachosema, wapo katikati ya kelele.
Njia rahisi ya kuvuka kelele hizo ni kupiga kelele zaidi, lakini hilo halitakusaidia kwa muda mrefu.
Kwa sababu kwanza utachoka haraka, halafu hutawafikia wengi kama unavyotaka, maana kuna ukomo wa kelele unazoweza kupiga.
Sehemu yoyote yenye wingi wa chochote kile, njia bora ya kusimama ni kuwa tofauti.
Sehemu yoyote yenye kelele nyingi, njia pekee ya kusikika na wale unaotaka wakusikie ni kuwa tofauti.
SOMA; UKURASA WA 100; Usipige Kelele, Fanya Watu Waone…
Kuwa tofauti na hutahitaji kupiga kelele, kwa sababu wale wanaotaka unachotoa, wanaotaka kusikia unachosema, wanajua wapi tofauti wanaweza kukupata wewe.
Inashawishi sana kutaka kupiga kelele zaidi ya wengine, maana utakapoanza kufanya hivi, utaona matokeo mazuri mwanzoni, lakini baadaye matokeo hayo yatapungua na kadiri unapiga kelele hakutakuwa na matokeo mazuri tena.
Kuwa tofauti, angalia kipi wengine hawawezi kufanya na fanya wewe, angalia wapi wengine hawaendi na nenda wewe.
Kitu pekee kinachoweza kukutofautisha kwenye zama hizi za kelele ni kuweka kazi kubwa, maana wapiga kelele wengi huwa hawawezi kufanya kazi kubwa. Kama utaacha kupiga kelele na ukaweka kazi, utajitofautisha na wengi na utaweza kupiga hatua kubwa.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,