Kwenye hii dunia, kuna makundi mawili ya watu,
Kundi la kwanza ni wazalishaji, hawa ni wale wanaofanya mambo yatokee, wanaozalisha vitu, mawazo au kutoa matokeo fulani ambayo watu wanayatumia kwenye maisha yao. Wazalishaji wanaleta kitu pasipo na kitu, wanaleta uwezekano pasipo na uwezekano, na wanawapa watu wengine kitu cha kufanya au kutumia.
Kundi la pili ni walaji, hawa ni wale wanaotumia vitu vilivyozalishwa na wazalishaji, wale wanaopokea matokeo yaliyotolewa, wanaofuata kile ambacho kimefanywa na wengine. Walaji wanachukua kile kinachotolewa na wazalishaji, na kukitumia kwenye maisha yako.
Sasa kwenye maisha kila mtu ana nafasi ya kuwa kwenye pande hizi mbili, kila mtu kuna vitu anazalisha na pia kuna vitu anatumia kutoka kwa wengine wanaozalisha.
SOMA; UKURASA WA 970; Hamasa Haisubiriwi, Hamasa Inatengenezwa…
Lakini kwenye maisha, kuna tofauti kubwa sana kwa mtu, wakati anazalisha na wakati anatumia kilichozalishwa na wengine. Wakati mtu anazalisha, anajisikia vizuri, anaona jinsi anavyokuwa mchango kwa wengine kuchukua hatua, anaona anachotoa jinsi kinayafanya maisha ya wengine kuwa bora zaidi.
Kwa upande wa ulaji, hakuna furaha kubwa kwenye ulaji, hata kama kitu ni kizuri kiasi gani, baada ya muda watu wanazoea. Kadiri mtu anavyozidi kuwa mlaji, ndivyo anavyozidi kujisikia vibaya, kwa sababu ulaji hauna hamasa kubwa, na unapotumia zaidi vitu vya wengine, unazidi kujiona wewe ni tegemezi zaidi.
Hivyo rafiki yangu, kama kwa namna yoyote unajisikia vibaya, kama unasikia kuna kitu hakijakamilika ndani yako, zalisha kitu. Ukizalisha kitu, unabadili kabisa fikra zako, utaondoka kwenye kujisikia vibaya na utaenda kujisikia shujaa, utajiona wa muhimu na mwenye mchango kwa wengine.
Mara zote hakikisha kuna kitu unazalisha, hili litakuwezesha kuwa na hamasa kubwa wakati wote.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,