Kwenye biashara yako, utakutana na wateja wengi wanaotaka uwapunguzie bei. Sasa kama bei zako umepanga kwa usahihi, kwa kuzingatia thamani ambayo wateja wanaipata, hupaswi kupunguza bei.
Kwa sababu tabia ya kupunguza bei ina madhara makubwa kwenye biashara yako kwa baadaye, hata kama unaona kwa sasa ina manufaa.
Mara kwa mara utakutana na wateja watakaokuambia kwamba bei zako ziko juu sana. watakuambia wengine wanauza kwa bei ndogo kuliko unavyouza wewe.
Sasa wafanyabiashara wengi wanaposikia kauli hiyo, huwa wanachukua hatua moja kati ya hizi mbili;
Moja wanamuuliza mteja anauziwa kwa bei gani kwa wengine kisha nao wanapunguza bei na kumuuzia kwa bei hiyo.
Mbili wanamwambia mteja nenda kanunue huko unakouziwa kwa bei rahisi.
SOMA; UKURASA WA 864; Usipunguze Bei, Ongeza Thamani…
Yote hayo siyo majibu sahihi kwa mteja wako, hayamsaidii yeye wala hayakusaidii wewe.
Jibu sahihi pale mteja anapokuambia bei zako ni ghali, ni kumweleza thamani kubwa atakayoipata kwa kununua kwako kwa bei juu badala ya kwenda kununua kwa wengine kwa bei rahisi.
Hapo unaeleza thamani kubwa anayopata, ubora wa bidhaa na huduma anayopata na kwa jinsi gani akinunua kwa bei rahisi atahitaji kununua tena na tena ukilinganisha na kama atanunua kwako kwa bei ghali.
Kama unaijua biashara yako vizuri, unaijua shida ya mteja wako vizuri na unawajua washindani wako vizuri, hasa wale wanaouza kwa bei rahisi, utaweza kutengeneza wateja wazuri sana kwako.
Kwa sababu mtu yeyote anayeuza kwa bei rahisi hawezi kutoa huduma bora, kwa sababu faida anayopata ni ndogo sana. Lakini wewe unayeuza kwa bei ya juu, unaweza kutoa huduma bora na hivyo kuvutia wateja sahihi.
Faida nyingine ya kuuza kwa bei juu ni kuondokana na wateja wasumbufu, wale wateja wanaoangalia bei tu na siyo ubora. Hao waache wakawatese washindani wako, ili wewe upate nafasi nzuri ya kuwahudumia wateja bora kwako.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,