Nimewahi kukuambia usifanye mabadiliko makubwa kwenye biashara yako kwa sababu ya maoni ya mteja mmoja.
Maana kumekuwa na tabia ya wafanyabiashara kukata tamaa au kupata hamasa kubwa kwa sababu ya maoni ya mteja mmoja au wachache.
Wanakata tamaa pale mteja anapowaambia kwamba wanachouza hakifai au siyo wanachotaka, hivyo wanaona ndiyo mtazamo wa wateja waote na kuamua kuacha.
Pia wanapata hamasa pale mteja mmoja au wachache wanawaambia kuna kitu wanataka ambacho wao hawana. Wanahamasika sana kuwa na kitu hicho wakiamini ndiyo hitaji halisi la wateja.
Unahitaji kuwa makini sana unapofanya maamuzi makubwa kwenye biashara yako, kama ya kuacha kuuza kitu fulani au kuanza kuuza kitu fulani. Kwa sababu maoni ya mteja mmoja au wachache haimaanishi ndiyo maoni ya wateja wako wote.
Jua kwamba wateja wote wa biashara yako hawafanani, na pia wateja hawapo vile vile kila siku. Wateja wanabadilika kulingana na mambo yanavyobadilika kwenye maisha yako.
SOMA; Aina tatu za wateja na jinsi ya kufanya nao biashara.
Kuna wateja ambao wanajua nini wanataka na wapo tayari kulipia ili kupata wanachotaka. Hawa ni wateja ambao ukikutana nao unapata hamasa sana, na kama ukikutana nao mwanzo wa biashara, unaweza kuwa na mategemeo makubwa sana kwenye biashara yako. Lakini sivyo wateja wote walivyo.
Kuna wateja ambao hawajiamini na hivyo hawakuamini wewe na biashara yako. Wanaamini kila mfanyabiashara ni mwizi na anapata faida kubwa kwa kuwanyonya wateja wake. Ukikutana na wateja hawa wengi unaweza kutamani kuondoka kwenye biashara.
Kuna wateja ambao wanaangalia bei tu, wanakazana sana uwauzie kwa bei ya punguzo, na hata baada ya kuwapunguzia wanaendelea kukusumbua mno. Hawa ni wateja ambao wanaamini wakilipia kitu basi wanapata mamlaka ya kumtesa yule waliyemlipa. Hivyo ikitokea shida kidogo wanakuja kwako, hata shida ambayo wangeweza kutatua wenyewe.
Jua tabia mbalimbali za wateja wako, na haijalishi tabia ni nzuri au mbaya kiasi gani, jihakikishie tu kwamba siyo kwamba wateja wote wako hivyo. Hivyo kukatishwa tamaa au kuhamasishwa na mteja mmoja haimaanishi ndivyo wateja wote walivyo.
Jua biashara unayoifanya, jua changamoto za wateja unazotatua na kazana kutoa thamani kubwa. Kila wakati kazana kuboresha zaidi kadiri unavyoona inafaa na inahitajika. Na zijue vizuri tabia za wateja wako ila usikubali zikuyumbishe.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,