Unapoangalia hapo ulipo sasa na kule unakokwenda, kuna nafasi kubwa, kuna pengo kubwa ambalo unapaswa kuliziba ili kufikia yale maisha unayoyataka.

Kuna njia mbili za kuangalia nafasi hiyo unayopaswa kuivuka ili kufikia maisha unayoyataka.

Njia ya kwanza ni kuangalia pengo ambalo lipo kutoka ulipo sasa mpaka kufika kule unakoelekea. Hii ni njia ambayo itakuonesha kipi ambacho bado hujafanya. Ni njia nzuri ya kuhamasisha, lakini kama pengo ni kubwa, inaweza kuwa njia ya kujikatisha tamaa. Kwa sababu utaona ni vigumu kuvuka pengo hilo.

Njia ya pili ni kuangalia hatua ambazo tayari umeshapiga, hapa unaangalia nyuma kabisa ulikotoka na hatua ambazo umeshachukua mpaka hapo ulipofika sasa. Hii ni njia nzuri ya kukuonesha kwamba tayari umeshafanya makubwa hivyo kuacha, ni kupoteza yote uliyoyafanya.

SOMA; UKURASA WA 230; Kipimo Cha Kujua Kama Kweli Unafanya Kile Ulichokusudiwa Kufanya.

Ili kupata hamasa ya kufika popote unapotaka kufika, ili kuweza kutoka ulipo sasa na kufika mbali unakoelekea, ni bora kuangalia zaidi hatua ulizopiga kuliko kuangalia pengo lililobaki.

Kila unapokutana na magumu, kila unapokutana na kushindwa na kila unapokutana na hali ya kukukatisha tamaa, angalia kwanza wapi umetoka, angalia hatua ambazo mpaka sasa umeshapiga. Hii itakuonesha kwamba pamoja na magumu, kuna kitu umefanya.

Angalia pengo lililobaki pale tu unapopitia mipango yako na kuweka mikakati ya kupiga hatua zaidi. Lakini wakati mwingine, angalia hatua ambazo tayari umeshapiga, na utapata hamasa ya kuchukua hatua zaidi.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha