“The aim of life is self-development. To realize one’s nature perfectly—that is what each of us is here for.” — Oscar Wilde

Hongera sana mwanamafanikio kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni nafasi bora na ya kipekee kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora.
Kwa msingi wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa TATUA, AMUA NA ONGOZA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.

Asubuhi ya leo tutafakari KUSUDI KUU LA MAISHA…
Kusudi kuu la maisha ni kujiendeleza binafsi.
Na hili halina mwisho,
Kwa sababu haijalishi umepiga hatua kiasi gani, bado kuna hatua zaidi unaweza kupiga.
Haijalishi umepanda juu kiasi gani, bado unaweza kupanda zaidi.
Na pia haijalishi unajua kiasi gani, bado kuna mengi zaidi unahitaji kujua.

Japokuwa hakuna ukamilifu kwenye maisha, lengo lako la kila siku linapaswa kuwa kusogea karibu zaidi na ukamilifu.
Kila siku inapaswa kuwa bora kuliko jana,
Hivyo kama unaona afadhali ya jana, jua leo umepotea.
Na kama unaona leo ni kama jana, hakuna jipya jua unabaki nyuma.

Kuwa tayari kujifunza kila siku,
Kuwa mnyenyekevu,
Na kuwa tayari kujaribu vitu vipya kila siku.
Usiogope hatari, usiogope kushindwa, usisikilize hofu.

Lengo kuu la maisha yako ni kupiga hatua zaidi kila wakati,
Nenda kapige hatua leo zaidi ya ulivyopiga jana.
Nenda kajifunze leo tofauti na ulichojifunza jana.

Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kocha