Moja ya sababu kubwa kwa nini kila mmoja wetu anapaswa kuwa na orodha ya vitu atakavyofanyia kazi kwenye siku yake ni kwamba siku inavyoharibika huwa siyo rahisi kuonekana.

Unachoshangaa ni siku yako imeisha, umechoka, lakini ukiangalia, hakuna kikubwa umefanya, hakuna matokeo mazuri uliyozalisha.

Tunazungukwa na kila aina ya usumbufu, na usumbufu mkubwa kuliko wote tunatembea nao popote tunapoenda, ambao ni simu zetu. Na pale simu inapokuwa ina mitandao ya kijamii, na kila kinachoendelea kwenye mitandao hiyo unapata taarifa, basi siku yako inaweza kuwa imevurugwa kuliko hata siku ya vita.

Ni muhimu sana kujilinda ili usinase kwenye yale yasiyo muhimu, kwa sababu ni rahisi sana kunasa.

Kwa mfano, umewahi kusema unaingia kwenye mitandao ya kijamii kwa dakika chache ili uone nini kinaendelea, lakini ukastuka umeshatumia muda mwingi kuliko ulivyopanga?

Ni kwa sababu mitandao hiyo imetengenezwa kama kasino. Kwa sababu ndani ya kasino huwa hakuna saa, na kuna mwanga fulani muda wote, hivyo unaona kama muda hauendi, ukistuka n asubuhi.

SOMA; UKURASA WA 499; Dawa Ya Usumbufu Wa Mitandao…

Kadhalika mitandao ya kijamii, imetengenezwa kukuweka pale muda wote. Kila ukitaka kutoka unajiambia kuna kingine cha kuona, labda ukishuka chini zaidi utaona vizuri zaidi.

Na mitandao mingine ukitaka kutoka inakuonesha vitu ambavyo bado hujaona, hivyo unakuwa kama unaanza tena.

Wito wangu kwako rafiki yangu, jikinge sana na kila aina ya usumbufu. Jua nini unataka na maisha yako, weka vipaumbele vya siku yako na kaa mbali na mitandao ya kijamii na hata simu yako wakati wa kazi.

Weka ukuta baina yako na kile kinachoendelea kwenye maisha ya wengine, ili uweze kupata muda mzuri wa kuweka kwenye kazi unayofanya na upate matokeo bora.

Usiruhusu umakini wako, nguvu zako na muda wako vipotelee kwenye mambo yasiyo muhimu zaidi kwako.

Kama bado unahitaji kufuatilia nini kinaendelea, tenga muda mfupi wa kufuatilia hayo na uwe mwisho wa siku, pale ambapo tayari umeshakamilisha majukumu muhimu ya siku yako. Isiwe mwanzo wa siku au katikati ya majukumu yako muhimu.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha