Kosa moja wanalofanya wafanyabiashara wengi ni kuanzisha biashara zao kwa kujifikiria wao wenyewe, au kuangalia wafanyabiashara wengine wanafanya nini.

Biashara yoyote inayoanzishwa na mtu kwa sababu anafikiria ananufaikaje na biashara hiyo pekee, au kwa kuwaangalia wengine wanaofanya biashara hiyo na kujiambia inalipa ndiyo maana wapo, lazima biashara hiyo ishindwe.

Biashara ya aina hiyo inashindwa kwa sababu inakuwa imeruka hatua moja muhimu sana kwenye kuanzisha na kukuza biashara ambayo ni mteja. Kama unaanza biashara yako bila ya kumfikiria mteja, unajiandaa kushindwa.

Mipango yoyote unayofanya kwenye biashara yako, mtu pekee wa kuanza kufikiriwa ni mteja wa biashara hiyo.

Na hapa ndipo dhana ya mteja wa mfano inapokuja. Kila biashara inapaswa kuwa na mteja wa mfano. Hapa unachagua mtu wa kufikirika, ambaye unamfikiria kama mteja wa biashara yako.

Mtu huyo anakuwa na tabia ambazo zinaendana na biashara yako.

Mtu huyo anakuwa na mahitaji au shida ambayo inatatuliwa na biashara ambayo unaifanya wewe.

Mtu huyo anakuwa anapatikana eneo ambalo biashara yako inaweza kumfikia.

Na mtu huyo anakuwa na uwezo wa kumudu kulipa kile ambacho biashara yako inamtaka alipe.

Huyu ndiye mtu unayepaswa kumfikiria kila wakati, na mabadiliko yoyote unayofanya kwenye biashara yako, lazima kwanza yamwangalie mtu huyu.

Unaweza kuchagua wateja wachache wa biashara yako, na ukawa unawafikiria hao mara nyingi. Lakini kwa kuwa wateja hawafanani, unahitaji kutengeneza mteja wa kufikirika, ambaye utampa sifa na mahitaji mengi, kiasi kwamba sehemu kubwa ya wateja wako wanaangukia kwenye baadhi ya sifa za mteja wako wa mfano.

Usifanye maamuzi yoyote ya biashara kwa kujifurahisha wewe mwenyewe au kwa sababu wengine wanafanya maamuzi ya aina hiyo. Kabla hujafanya maamuzi yoyote anza kumfikiria mteja wako wa mfano kwanza. Je maamuzi unayofanya yatamsaidiaje awe bora zaidi? Je yatamwezeshaje kujihusisha na biashara yako zaidi?

Ukifikiria hivi kila mara, biashara yako itaendelea kupiga hatua zaidi na zaidi.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha