AMKA mwanamafanikio,
Amka kwenye siku hii nzuri na ya kipekee sana kwetu.
Ni siku ambayo tumepata nafasi nzuri ya kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.

Kwa msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa TATUA, AMUA NA ONGOZA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.

Asubuhi ya leo tutafakari UKISHAPANGA TEKELEZA…
Sababu pekee kwa nini tunaweka mipango kabla ya kuanza kitu, ni ili tuwe na kitu tunachofuata kwenye ufanyaji.
Kwa sababu usipokuwa na mipango, hutajua unafanya kiasi gani na huwezi kupima ufanyaji wako.

Pia usipokuwa na mipango, ni rahisi kuishia njiani ukifikiri umefanya sana kumbe hujafanya kama unavyodhani.
Ni muhimu sana kupanga kabla hujaanza kufanya. Kwa sababu mipango yako itakuwa mwongozo kwako.

Lakini pia kuna tatizo moja kwenye kupanga,
Wengi wanapanga, lakini hawatekelezi.
Inapofika wakati wa kutekeleza, wanakuwa na sababu nyingi kwa nini hawatekelezi.
Au wanaanza kidogo na wakikutana na kikwazo wanaacha kufanya.

Rafiki, nataka ufanye azimio moja na nafsi yako,
Chochote unachopanga kitekeleze.
Unapofika muda uliopanga kufanya, acha vingine vyote ma fanya.
Na hata kama utakutana na ugumu, usiache kufanya mpaka ule muda uliopanga kwamba utafanya ukamilike.

Hata kama unaumia, hata kama inakugharimu kwa ziada, hata kama itakubidi usilale au usile, ulipanga mwenyewe, sasa fanya.
Hii itakisaidia sana, unapofanya kila unachopanga, unajiheshimu na inakiwa rahisi kwako kufanikiwa.
Lakini unapopanga mwenyewe halafu hufanyi, unaanza kujidharau, unajiona siyo mtu makini, unazidi kushindwa kufanya na mwishowe unaacha kabisa kupanga kwa sababu unaona umekuwa unajidanganya kwenye mipango yako.

PANGA, KISHA TEKELEZA KILE ULICHOPANGA, BILA YA KUJALI INAKUGHARIMU AU KUKUUMIZA KIASI GANI.

Uwe na siku bora sana leo, siku ya kutekeleza kila ulichopanga.
#Fanya #HakunaSababu #NiLeoTu #IngiaMzimaMzima #AnzaNaHatuaMoja #MafanikioNiHakiYako #NidhamuMsingi #WhatEverItTakes #WachaManenoWekaKazi #SkinInTheGame #OwnTheDayOwnYourLife #UsileteSababuLetaMatokeo #MudaNiSasa

Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kocha