Ukiona giza limekuwa nene sana jua pamekaribia kupambazuka, hii ni kauli ya waswahili inayoashiria kwamba pale mambo yanapoonekana ni magumu zaidi, ndiyo karibu na ushindi.

Na huu ndiyo uhalisia wa maisha, pale mtu anapofikia mwishoni kabisa mwa jambo lolote, yaani anakaribia kupata matokeo makubwa sana, ndiyo mambo huwa yanaonekana ni magumu kuliko wakati wowote ule.

Hapo mwishoni ndiyo hatari inaonekana kubwa na isiyoweza kubebeka. Na hapa ndipo wengi huishia, kwa kukata tamaa na kuona hawawezi kuendelea tena. Wasijue ni karibu kiasi gani na matokeo makubwa walikuwa wamefika.

Ni kama asili inatupima, kutaka kujua tumejitoa kiasi gani, kutaka kujua tupo tayari kiasi gani kupata kile tunachotaka. Ni wale wachache wanaovuka hatua hiyo ngumu ndiyo wanakutana na mafanikio makubwa upande wa pili.

Cha kujifunza hapa rafiki yangu ni hichi muhimu sana, unapochagua kufika hatua fulani kwenye maisha yako, jitoe kuweka juhudi mpaka ufikie hatua hiyo. usikubali kuishia njiani, hata kama mambo yatakuwa magumu kiasi gani, usijaribu hata kidogo kukata tamaa.

Pale unapojiambia kwamba mambo yamekuwa magumu sana na huwezi tena, jua ndiyo wakati sahihi kwako kuendelea, kwa sababu unaweza kuwa upo karibu sana na ushindi kuliko unavyotegemea.

Na kila unapokutana na ugumu mkubwa kwenye maisha yako, jua unakaribia ushindi mkubwa sana kama hutakata tamaa.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha