Tunapohitaji kushirikiana na wengine kwenye safari yetu ya mafanikio, huwa tunasahau kwamba wale ni watu kama sisi.
Huwa tunasahau hilo na kuona labda ni watu wasioeleweka au wasioweza kutuelewa au kufanya kile tunachotaka.
Tunasahau kwamba ni watu kama sisi, ambao wana mahitaji kama ambavyo tunayo sisi, ila tu yanatofautiana kwenye aina ya mahitaji na kiwango cha mahitaji hayo.
Ili kuimarisha mahusiano na ushirikiano wako na wengine, unahitaji kujua ni nini wanataka kisha kuwapa. Unahitaji kujua wanajali nini zaidi na kuwapa hicho.
Mahusiano yetu kwenye maisha ni nipe nikupe, unaweza kupata kile unachotaka kama utawapa wengine kile ambacho wanataka.
Hivyo jukumu lako la kwanza ni kujua watu wanataka nini na kuwapa, na wao watakuwa tayari kukupa kile unachotaka.
Jua watu unaotaka kushirikiana nao, unaotaka kuwauzia au unaotaka wakusaidie kitu fulani, ni watu ama wewe ambao wana mahitaji yao kama ulivyo na mahitaji yako wewe.
Jinsi unavyowatendea vizuri watu, ndivyo nao wanavyokutendea vizuri pia. Hivyo yeyote unayekutana naye, usimchukulie tu kama mteja, mfanyakazi au mhudumu wako. Bali mchukulie kama mtu mwenye mahitaji yake, ambaye kama utamsaidia apate mahitaji hayo, atakusaidia na wewe kupata kile unachokitaka.
Ni watu kama wewe, watendee vile ungependa wakutendee na mahusiano yako yatakuwa bora sana.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,