Mtu mmoja aliwahi kusema maneno makali sana kuhusu mitandao ya kijamii. Alisema kwa mitandao ya kijamii ambayo watu wanatumia bure, wasichojua ni kwamba wao watumiaji ndiyo bidhaa ambayo mitandao hiyo inauza.

Kwa sababu mitandao hiyo inaingiza fedha kwa njia kuu moja, ambayo ni matangazo. Na njia pekee wanayopata fedha kwenye matangazo ni kuuza taarifa zako kwa wale wenye uhitaji nazo.

Kwa mfano kama mtu anataka kuwatangazia wanaume, wenye miaka kati ya 25 mpaka 35 na wanaokaa eneo fulani, kama wewe ni mmoja wao basi taarifa zako zitauzwa kwa mtangazaji huyo na utaona aina hiyo ya tangazo.

Sasa hilo siyo tatizo kubwa, maana pia inaweza kukurahisishia kupata vitu unavyotaka.

Lakini ni tatizo, hasa pale watu wanaonunua taarifa zako wanapozitumia vibaya. Na kwa dunia hii ya kelele, kila mtu anagombania kupata umakini wake. Kila mtu anaweza kuahidi vitu ambavyo hata siyo kweli, ili kukuvutia tu usome, kusikiliza au kuangalia chochote anachotaka kukitumia kukushawishi.

Hivyo huu ni wakati wa kuwa makini sana na umakini wako, muda wako na yale ambayo ni muhimu kwako. Utakutana na wapiga kelele wengi, lakini kama wanachokupigia kelele siyo kitu muhimu, achana nao.

Usikubali kuwa mteja wa kila anayetaka kuuza chochote kwenye ulimwengu huu wa kelele. Chagua kuachana na kukataa vitu vingi na utaokoa muda wako na nguvu zako ambazo ungepoteza kwenye mambo yasiyo muhimu.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha