Rafiki yangu mpendwa,

Kila mmoja wetu ana masaa 24 pekee kwenye siku yake, hakuna mwenye uwezo wa kuongeza hata dakika moja kwenye siku yake.

Katika masaa hayo 24, wapo ambao wanaweza kufanya makubwa sana na kufanikiwa, na pia wapo wanaoshindwa kufanya na kuwa na maisha ya kushindwa.

Katika masaa hayo 24, wapo wanaofanya yale muhimu na maisha yao yanakwenda vizuri, na pia wapo ambao wanaishia kulalamika hawana muda wa kutosha kufanya kila wanachotaka kufanya.

Kwa kifupi, muda ndiyo kitu pekee ambacho watu wote tumepewa sawa, na ndiyo kitu pekee kinachoweza kupima kama tutafanikiwa au la.

Watu wanaofanikiwa, wanathamini sana muda wao kuliko hata fedha. Kwa sababu wanajua wakipoteza fedha wanaweza kuzipata tena, ila wakipoteza muda hawawezi kuupata tena. Hivyo wanalinda sana muda wao na wanakuwa na vipaumbele kwenye kila dakika ya maisha yao.

Lakini kwa wale wanaoshindwa, muda ni kitu ambacho wanajiuliza wakipotezeje, maana hawajui thamani yake. Yaani utakutana na mtu anakuambia kabisa nipo napoteza poteza muda hapa. Utawakuta wanafanya vitu vya hovyo na muda wao, na wanachagua kupoteza muda wao kama vila hauna maana yoyote kwao.

Rafiki yangu, nilishakushirikisha JINSI YA KUPATA MASAA MAWILI KILA SIKU, unaweza kujua zaidi kwa kubonyeza hayo maandishi.

MASAA MAWILI YA ZIADA

Leo nakwenda kukushirikisha saa moja muhimu sana kwenye maisha yako, ambayo ukiweza kuilinda saa hiyo vizuri na kuitumia kwa yale muhimu, kila siku kwako itakuwa siku ya mafanikio sana.

Waandishi wengi sana wameandika kuhusu umuhimu wa saa hii ninayokwenda kukushirikisha leo, hivyo ni kitu unachopaswa kukizingatia kwa uzito wa hali ya juu sana, kwa sababu itakusaidia sana.

Saa moja muhimu sana kwenye kila siku ya maisha yako, ni lisaa limoja la kwanza kwenye siku yako. Yaani ule muda ambao unaamka, na saa moja tangu umeamka, ndiyo muda muhimu sana kwenye kila siku yako.

Kama huwa unaamka saa kumi asubuhi, basi saa kumi mpaka saa kumi na mja asubuhi ni saa moja muhimu sana kwenye maisha yako. Kadhalika kama unaamka saa 11 asubuhi, saa 11 mpaka saa 12 ni muda muhimu. Na hata kama unaamka saa tatu asubuhi, saa tatu mpaka saa nne ni muda muhimu sana kwako.

Saa moja tangu unapoamka unapaswa kufanya kuwa muda mtakatifu kwako, muda ambao unapaswa kuudhibiti kwa asilimia 100 na kutokuupoteza kwa kitu chochote kile.

Waandishi wengi wanatuambia kwamba ukiweza kudhibiti saa moja ya kwanza kwenye siku yako, utaweza kuyadhibiti maisha yako na ukiweza kufanya hivyo kila siku, basi utaweza kuwa na mafanikio makubwa sana kwenye maisha yako.

Vitu unavyopaswa kufanya kwenye saa moja ya kwanza ya siku yako.

 1. Andika malengo yako makubwa kwenye maisha, malengo ya siku, wiki, mwezi, mwaka na ya maisha.
 2. Andika mipango unayokwenda kufanyia kazi kwenye siku hiyo, na pangilia muda wa siku nzima utakavyoutimia.
 3. Soma kitabu au sikiliza au kuangalia mafunzo yanayokufundisha na kukuhamasisha.
 4. Sali na/au fanya tahajudi.
 5. Fanya mazoezi.
 6. Fanya kile muhimu zaidi kwenye maisha yako, kama kuandika, kujifunza kitu unachofanyia kazi na kadhalika.

Vitu unavyopaswa kuepuka kufanya kwenye saa moja ya kwanza ya siku yako.

 1. Usitumie simu kwenye saa moja ya kwanza ya siku yako.
 2. Usiingie kwenye mitandao ya kijamii au barua pepe.
 3. Usiangalie, kusikiliza au kusoma habari ya aina yoyote ile.
 4. Usiingie kwenye usumbufu wa aina yoyote ile kwenye muda huu.
 5. Usipoteze muda huu kufikiria ufanye nini au kuwa upo upo tu na huna unachofanya.

Rafiki yangu, saa moja ya kwanza kwenye kila siku yako, ni siku unayopaswa kuimiliki kwa asilimia 100 na usiruhusu yeyote aingilie saa hii.

Na hata kama unajiambia upo bize kiasi gani, umebanwa kiasi gani, unahitaji kutenga na kulinda saa hii muhimu sana kwa maisha yako.

Usikubali watu wachukue na kumiliki masaa yote 24 ya kila siku yako.

Hivyo kama ukiamka asubuhi inabidi uwahi mahali fulani, labda kazini au kwenye biashara, utahitaji kuwahi kuamka zaidi ili upate muda wako wa saa moja kwenye kila siku yako.

Nakusisitiza sana kwenye hili rafiki kwa sababu najua umuhimu wa saa hii muhimu. Mimi ni shahidi mzuri wa saa hii, na mimi nina masaa mawili matakatifu kwenye kila siku yangu. Kuanzia saa 10 asubuhi mpaka saa 12 asubuhi ni muda nilioutenga kwa ajili yangu na kwa ajili ya kazi muhimu ya uandishi. Ni katika muda huu ndiyo nimekuwa nakuandalia makala mbalimbali ninazokushirikisha.

Hivyo rafiki, tenga muda ambao utakuwa unaamka, saa moja kabla hujahitaji kufanya yale uliyozoea kufanya, na tumia saa hiyo moja kwa yale muhimu sana kwako.

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali. Kupata Huduma Za Ukocha Tembelea; www.amkamtanzania.com/kocha

Usomaji