Kila mara jina lako linapotajwa kwa watu, ukiwa haupo, kila mtu kuna picha ambayo anaijenga kwenye akili yake kuhusu wewe.
Sasa wengi wamekuwa wakijaribu kujenga picha fulani kwa nje, ambayo imekuwa haifanikiwi.
Kwa zama hizi za mitandao ya kijamii, kila mtu anaweza kuwa muigizaji wa maisha, akitengeneza picha ya nje ambayo watu wanaweza kufikiri ni mtu wa aina fulani.
Lakini ndani yake, unakuta ni mtu tofauti kabisa na ile picha ya nje anayoonesha.
Swali langu kwako leo ni je unajulikana kwa kipi? Pale jina lako linapotajwa, watu wanapata picha gani?
Kama watu wanapata picha ambayo ni tofauti na ulivyotarajia, basi jua kuna namna unaigiza maisha.
Kwa sababu, watu wanajenga picha juu yetu kulingana na jinsi ambavyo tumegusa maisha yao. Hivyo watu wanaweza kutupenda na kutuamini kwa namna tumeyagusa maisha yao kwa ubora. Na pia watu wanaweza kutuchukia na kutokutuamini kwa namba ambavyo tumeyavuruga maisha yao.
Unachohitaji ili kujenga taswira nzuri kwa wengine, siyo kukazana na maigizo, bali kukazana kuishi maisha bora kwako na yanayogusa wengine kwa ubora.
Kila wakati angalia ni kwa jinsi gani unaweza kuongeza thamani kwenye maisha ya wengine. Na wao watachagua kukuamini na kukupenda, kwa sababu umegusa maisha yao kwa ubora.
Usipoteze muda wako kuigiza maisha, badala yake ishi maisha yenye uhalisia kwako na yenye msaada kwa wengine.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,