Nimekuwa nasema hili na bado naona wengi hawalipati vizuri. Watu wengi wanaingia kwenye biashara kwa sababu ambazo siyo sahihi, na hilo linawaumiza sana. Watu wanakuwa na mategemeo fulani wanapoingia kwenye biashara, lakini wakiingia wanakutana na uhalisia tofauti ambao unawaumiza sana.
Watu wanaingia kwenye biashara wakiamini watakuwa na uhuru na muda na maisha yao kwa namna wanavyotaka wao. Ni mpaka pale biashara inapoanza kukua ndiyo wanagundua biashara inawahitaji kuliko walivyofikiri.
Wengine wanafikiri wakiingia kwenye biashara watakuwa na furaha, kwa sababu wanafanya maamuzi yao wenyewe. Ni mpaka pale wanapokutana na uhalisia kwamba kwenye biashara kila siku ni kazi ya kuzima moto, kila siku kuna changamoto za kutatua na kipato chenyewe siyo cha uhakika, leo juu, kesho chini ndiyo wanagundua kuingia kwenye biashara siyo sehemu ya kupata furaha.
Wapo wanaoingia kwenye biashara wakiamini ndiyo njia ya haraka ya kufika kwenye utajiri na uhuru wa kifedha. Ni pale wanapokaa kwenye biashara kwa zaidi ya miaka miwili na wakiangalia kitu pekee walichoweza kufanya ni kuzuia biashara isife, ndiyo wanagundua hakuna njia ya mkato kwenye biashara.
Rafiki, kitu pekee ambacho unaweza kukitegemea kwenye biashara, ni juhudi unazochagua kuweka, matatizo unayochagua kutatua na wateja unaochagua kuwahudumia.
Sasa ukishajua hayo, na kuweka juhudi zako, nguvu zako na muda wako wote kwenye maeneo hayo, huna haja ya kujali kuhusu uhuru, muda na hata fedha. Kadiri unavyokuwa bora kwenye maeneo tuliyotaja hapo juu, ndivyo unavyopata kila unachotaka.
Ila kumbuka hili vizuri, juhudi zinahitajika, muda unahitajika, kazi kwa sana na uvumilivu.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,