Moja ya vitu vinavyotusaidia sisi binadamu na hata viumbe wengine kuendesha maisha yetu kwa urahisi ni tabia.
Unapofanya kitu kwa mara ya kwanza, kinakuwa kigumu kwako, kwa sababu unahitaji kufikiria kila hatua kwenye ufanyaji. Lakini kadiri unavyoendelea kufanya, hatua nyingi zinakuwa ni za kujirudia, na hivyo tabia inajengeka ndani yako.
Ndani ya muda mfupi unajikuta unafanya kitu bila hata ya kufikiria kabisa, yaani mwili unakuwa kama umeshazoea kiasi kwamba unaweza kufanya hata kama umelala.
Chukulia mfano wa kuendesha gari au hata baiskeli. Unapokuwa unaanza, kila hatua unaifikiria na hivyo linakuwa zoezi gumu sana. Kushika breki ni mpaka ufikirie, kuweka gia mpaka ufikirie, kila hatua inakuwa zoezi gumu.
Lakini baada ya kuzoea, unajikuta unaendesha umbali mrefu bila hata kujua saa ngapi umeweka gia au kushika breki.
Kadiri tabia nzuri zinavyofanya maisha yetu kuwa rahisi, ndivyo tabia mbaya zinavyofanya maisha yetu kuwa magumu, na hata kuziondoa inakuwa ngumu sana.
Kwa sababu mpaka kitu kinakuwa tabia, kinakuwa kimeshaondoka kwenye fikra zetu za kawaida na kwenda kwenye fikra za ndani kabisa. Hizi ni fikra ambazo zinafanya bila ya sisi kuzidhibiti.
Sasa kama tabia inafanyika bila ya wewe kufikiri, kwa nini unadhani unaweza kuiondoa au kuibadili kwa kufikiri? Ni vigumu sana kubadili kitu kwa njia ambayo hakifanyiki.
Hivyo njia pekee ya kubadili tabia ambayo imeshajijenga ndani yako, ni kubadili kabisa mfumo wa maisha yako kwa upande wa tabia hiyo. Kwa sababu mpaka tabia inajengeka, mwili umeshapewa viashiria kwamba kikitokea kitu hiki, basi kinachofuata ni hiki.
Mfano umeshajijenga tabia kwamba ukikasirika basi unatumia kilevi, au ukipata fedha basi unaanza kutumia.
Sasa ili kuondokana na tabia yoyote ile, lazima ujue mnyororo mzima wa tabia hiyo na uanze kuvunja mnyororo huo. La sivyo hutaweza kuondokana na tabia hiyo.
Mnyororo wa tabia huwa una vitu vitatu, kichocheo cha tabia, tabia yenyewe na zawadi baada ya tabia. Hivyo unapohitaji kubadili tabia, unahitaji kuanza kwenye kichocheo, lazima ujue ni nini kinakuchochea kufanya tabia hiyo. Pia unahitaji kuangalia zawadi ambayo unaipata ukitekeleza tabia hiyo, na ukiweza kubadili zawadi hiyo, utaweza kubadili tabia.
Usibadili tabia pekee, bali badili kichocheo kinachokupeleka kwenye tabia na pia badili zawadi unayoipata kwa kutekeleza tabia hiyo na utaweza kubomoa tabia yoyote mbaya uliyonayo.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,