“Makes flame and brightness out of everything that is thrown into it.” – Marcus Aurelius
Ni siku nyingine mpya mwanamafanikio.
Siku ya kipekee sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Kwa msingi wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa TATUA, AMUA NA ONGOZA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari WASHA MOTO UTAKAOANGAZA KILA KITU…
Utakapoanza kupiga hatua kwenye maisha yako, watu watakushambulia.
Watakurushia kila aina ya maneno, sababu, mapingamizi na hata chuki.
Sasa wewe huhitaji kuhangaika na watu wa aina hiyo.
Badala yake, jukumu lako kubwa ni moja, washa moto mkubwa sana, kiasi kwamba kila kinachorushwa kwenye moto huo kinaishia kuangaza zaidi.
Hatua unazochukua ndiyo moto unaowasha.
Na yale ambayo wengine wanakurushia, yanapaswa kuunguzwa zaidi na moto huo na kuchochea moto zaidi, kiasi kwamba wale ambao walikuwa hawaoni moto huo ukiwaka wauone.
Kwenye maisha, kuna watu wanachagua kufanya vitu, halafu kuna watu wanachagua kuwachambua wanaofanya vitu. Wote wao kazini, chagua tu unataka kuwa upande upi wa kazi.
Kama ambayo kuna wachezaji wa mpira na wachambuzi wa mpira, wote wapo kazini.
Jukumu lako ni moja, washa moto mkubwa sana, kiasi kwamba chochote kinachorushwa kwenye moto huo kinachochea moto zaidi.
Hata mtu akimwaga maji, akiamini anazima moto huo, anashangaa moto ndiyo unazidi kulipuka zaidi na zaidi.
Endelea kuchukua hatua kubwa sana bila ya kujali nani nasema nini.
Ni wewe pekee unayejua wapi unapokwenda, hivyo kusimama kwa sababu kuna watu wana maoni tofauti, ni kujichelewesha.
Uwe na siku bora sana ya leo, siku ya kuwasha moto ambao hauzimwi na chochote, ambao unaunguza na kuangaza kila kinachorushwa kwenye moto huo.
#Fanya #HakunaSababu #NiLeoTu #IngiaMzimaMzima #AnzaNaHatuaMoja #MafanikioNiHakiYako #NidhamuMsingi #WhatEverItTakes #WachaManenoWekaKazi #SkinInTheGame #OwnTheDayOwnYourLife #UsileteSababuLetaMatokeo #MudaNiSasa
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kocha