Watu wengi hawajui zama zimebadilika sana, na siyo tu kwenye sayansi na teknolojia, bali pia kwenye mahusiano.
Sasa hivi hatuishi tena kwenye uchumi wa ujamaa au ubepari, bali tunaishi kwenye uchumi wa kujuana na wa huduma.
Tunaishi kwenye uchumi ambao watu wanaojuana wanajaliana. Watu wananunua kutoka kwa watu wanaowajua, kwa sababu wanajua wanajali maslahi yao. Hizi siyo zile zama za kuuza ili kupata faida, na mteja akishanunua basi hiyo ni juu yake, hujali tena kama alichonunua kimemfaa au la.
Tunaishi kwenye uchumi wa huduma, ambapo haijalishi kama unauza chakula, unauza chuma au unauza ardhi, kinachokubeba siyo unachouza, bali huduma unayotoa. Watu wananunua pale wanapopata huduma nzuri, kabla, wakati na hata baada ya kununua.
Elewa uchumi tunaoishi sasa na nenda nao kwa usahihi, ijenge biashara yako kwa mfumo wa kujuana, wewe kuwajua wateja wako vizuri na wao kukujua wewe vizuri. Pia kazana kutoa huduma bora kabisa, ambazo mteja wako hawezi kuzipata sehemu nyingine ila kwako tu.
Ni biashara yako, itengeneze kwa msingi ambao utakuwa imara na kuiwezesha kufanikiwa. Kujuana na huduma ni uchumi tuliopo sasa, utumie vizuri.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,