Mwandishi Simon Sinek, ambaye anaandika na kufundisha sana kuhusu uongozi, ana kitabu kinaitwa Leaders Eat Last, akiwa na dhana kwamba viongozi wazuri huweka maslahi ya wengine mbele kabla ya maslahi yao binafsi.
Na ukichukulia kwa dhana hiyo ya kula, imekuwa inaaminika kwamba viongozi ndiyo wa kwanza kula. Lakini viongozi wazuri, ni wale wanaokula mwisho, baada ya kuhakikisha kila mtu amekula. Na hii siyo kutaka kuonekana kwamba unajali, bali ni kujali kweli, ni kuwa na uhakika kwamba chakula kipo cha kuwatosha wote na yeye pia. Na kama hakitoshi, basi ni bora kiongozi pia akose kuliko kiongozi apate na wengine wote wakose.
Tabia hii ya uongozi ukiweza kuitumia kwenye maisha yako utaweza kufanikiwa sana. Unachohitaji ni kuwa mgumu kwako binafsi lakini kuwa mwepesi kwa wengine. Nenda hatua ya ziada kuyafanya maisha ya wengine kuwa rahisi zaidi.
Weka mafanikio ya wengine kuwa kipaumbele chako cha kwanza. Wape watu nafasi ya kupata kitu kwanza, kwa sababu unaamini kwenye utele na siyo uhaba. Unapokuwa kwenye nafasi ya kupata kitu na wengine wanakihitaji pia, wape wengine nafasi ya kupata kwanza.
Mnapokuwa kwenye mlango wawili, mpe mwenzani nafasi ya kuingia kwanza. Kama upo njiani na kuna mtu anataka kukatisha, mpe nafasi ya kukatisha kwanza. Kama mpo eneo ambalo lina uhaba wa vitu, wape wengine nafasi ya kupata kwanza.
Unachofanya siyo kujinyima au kujinyanyasa, bali kuamini kwenye wingi na utele, kuamini kwamba wengine wakipata na wewe utapata.
Wape wengine kipaumbele kwenye maeneo mbalimbali na wewe utapata fursa kubwa zaidi. Kama kiongozi, unajua utapata tu, wengine wakishapata.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,