“Don’t find fault. Find a remedy.” —Henry Ford

Hongera sana mwanamafanikio kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni nafasi bora na ya kipekee sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Kwa msingi wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa TATUA, AMUA NA ONGOZA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.

Asubuhi ya leo tutafakari USITAFUTE KOSA, TAFUTA SULUHISHO…
Ni rahisi sana kutafuta na kuona makosa, kwako na hata kwa wengine.
Ni rahisi sana kunyoosha vidole, kulalamika na kulaumu wengine pale chochote kinapotokea.
Lakini kujua na kulalamikia kosa pekee hakuna msaada, sana sana kunazidi kuleta hasira na kukata tamaa.

Lakini kama utaichukua nguvu ile ile unayotumia kutafuta makosa, na ukaiweka kwenye kutafuta suluhisho, utaweza kuja na masuluhisho mengi sana ndani ya muda mfupi.
Kila utakachokutana nacho kitakuwa na jawabu na hatua za kuchukua kama utakuwa mtu wa kutafuta suluhisho badala ya kutafuta makosa zaidi.

Kama kuna kitu hakipo sawa, na unajua hakipo sawa, nguvu zako unapaswa kuziwekeza kwenye kufanya kitu hicho kiwe sawa. Huu utakuwa uwekezaji sahihi wa nguvu zako, kuliko kuendelea kutafuta kosa na kulalamika au kulaumu.

Umeona kosa au upungufu, njoo na suluhisho. Siyo rahisi na ndiyo maana wengi hawapendi.
Unapokuja na suluhisho unakuwa umejiweka kwenye utatuzi wa tatizo uliloona, sasa wengi hawapendi majukumu ya aina hii, ndiyo maana wamekuwa wanakimbilia kwenye kulalamika na kulaumu, kuliko kuja na suluhisho watakalosimamia mpaka kitu kikae sawa.

Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kuja na suluhisho kwenye kila changamoto au kikwazo unachokutana nacho.
#Fanya #HakunaSababu #NiLeoTu #IngiaMzimaMzima #AnzaNaHatuaMoja #MafanikioNiHakiYako #NidhamuMsingi #WhatEverItTakes #WachaManenoWekaKazi #SkinInTheGame #OwnTheDayOwnYourLife #UsileteSababuLetaMatokeo #MudaNiSasa

Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kocha