Mpendwa rafiki yangu,

Ni asili yetu sisi binadamu kugombana, kupishana kauli, hakuna mtu ambaye anaweza kuishi bila kukerwa na watu. Kama tunaishi hatuwezi kuacha kukwazana kwa sababu kila mmoja ana maisha yake hivyo siyo kila mtu atapenda vile unavyoishi maisha uliyojichagulia.

Katika kila ugomvi unaotokea kila mtu anataka kuibuka kuwa mshindi yaani ugomvi ni kama vile mabishano hivyo hakuna anayetaka kuonekana ameshindwa katika mabishano na kila mtu anajiona yuko sahihi kwa namna hii ni ngumu kumpata mshindi katika ugomvi ila leo ninakwenda kukupa mbinu ya kushinda katika ugomvi wa aina yoyote ile unaoujua.

Rafiki, kama unataka kushinda katika ugomvi wa aina yoyote ule unatakiwa kufanya kitu kimoja tu ambayo kitaweza kukusaidia kuibuka na ushindi. Kitu hiko siyo kitu kingine bali ni kusamehe. Njia ya kushinda katika ugomvi wa aina yoyote ni kutumia mbinu hii ya kusamehe tu. Kusamehe ni ushindi.

wp-image-646651137

Msamaha unayeyusha hasira zote na kukufanya kuwa bora. Unapoamua kuchukua hatua ya kusamehe ni umeamua kutua mzigo, umeamua kwa makusudi kushinda ugomvi. Ukitaka kushinda ugomvi wewe amua kuyaachilia yote hapo, amua kuwa mshindi kwa kusamehe, endelea na maisha yako ndiyo njia rahisi ya kushinda ugomvi.

Hakuna kisasi kizuri ambacho unaweza kumfanyia adui yako kama kumsamehe, unapoamua kusamehe ni sawa na umeamua kuwa huru, unaamua kwa makusudi kabisa kumfutia deni mdeni wako. Tunaishi bila kusamehe ndiyo maana maisha yanakuwa magumu kwa sababu kuishi bila kusamehe kila siku ni mwanzo wa kujitengenezea sumu mwenyewe, unajiwekea sumu ya panya katika chakula chako huku ukitegemea adui yako afe.

SOMA; Jinsi Unavyojitesa Katika Gereza Ulilojichagulia Wewe Mwenyewe

Unapoamua kusamehe amua kweli kusamehe hii ndiyo mbinu ya kushinda aina zote za magomvi, magomvi katika jamii, familia, ndoa na mambo mengine yote kwa sababu kama unaishi lazima kila siku kuna watu watakukosea hivyo njia nzuri ya kushinda ugumvi huo ni kuamua kusamehe.

Hatua ya kuchukua leo, kusamehe ni ushindi. Je unataka ushindi? Amua kusamehe, shida ugomvi wowote kwa kutumia mbinu ya kusamehe ndiyo utaweza kuwa mshindi.

Hivyo basi, maisha yetu yanahitaji kusameheana kila siku. Kila siku kazi yako iwe ni kusamehe kwa sababu unapoendelea kuweka kumbukumbu ya maumizo moyoni anayeumia siyo mtu mwingine bali ni wewe mwenyewe. Amua kusamehe ili uwe huru na maisha yako yaendelee mbele.

Ukawe na siku bora sana ya leo rafiki yangu.

Rafiki na mwalimu wako,

Deogratius Kessy

0717101505/0767101504

deokessy.dk@gmail.com , kessydeo@mtaalamu.net

Unaweza kutembelea tovuti yangu kwa kujifunza zaidi kila siku na kupata huduma mbalimbali kama vile vitabu, kwa kutembelea tovuti  hii  hapa  www.mtaalamu.net/kessydeo .

Asante sana na karibu sana!