Kuna njia mbili za kuingia kwenye biashara.
Moja; unaweza kuanza na suluhisho, kisha ukatafuta tatizo ambalo suluhisho lako linatatua.
Mbili; unaweza kuanza na tatizo, kisha ukatafuta suluhisho ambalo linatatua tatizo hilo.
Njia zote ni sahihi, ila pale unapoanzia biashara chini, na ukiwa huna rasilimali za kutosha, unahitaji kuanza na tatizo na siyo suluhisho.
Ukiwa huna rasilimali za kutosha, unahitaji kuanza na tatizo, kwa sababu lipo wazi na huhitaji kuwashawishi sana watu kununua. Unakuja na suluhisho la tatizo ambalo tayari watu wanalo na wanakuwa tayari kulipa ili kupata suluhisho hilo.
Ukiwa na rasilimali za kutosha, unaweza kuanza na suluhisho, kisha ukatafuta tatizo la kutatua. Hapo unaweza kufanya tafiti na pia una muda na rasilimali za kuwashawishi watu kwa nini wanunue. Inachukua muda lakini ukishatengeneza soko, biashara inakua vizuri.
Nikupe mfano kwenye teknolojia ya mawasiliano.
Kabla ya kuwepo kwa simu za mawasiliano, watu walikuwa na tatizo la mawasiliano, hivyo ujio wa simu ulikuwa jawabu kwao na haikuwa vigumu kuwauzia watu simu.
Lakini ujio wa simu janja, yaani smartphone, haukuanza na tatizo, bali ulianza na suluhisho. Kabla ya kuwepo kwa simu janja, hakuna mtu amewahi kulalamika kwamba amekosa simu janja. Simu za kawaida zilikuwa zimeshafanya maisha kuwa rahisi. Lakini watu walifanya tafiti, wakaona simu janja ni kitu kitakachoweza kuwasaidia watu, japo watu wenyewe walikuwa hawajui kama wanahitaji. Wakaja na simu janja, wakazitengenezea mfumo mzuri wa masoko na sasa simu janja ni sehemu ya maisha ya kila mtu.
Jua ni wapi unapoanzia wewe, na mara nyingi kazana kuanza na tatizo ambalo watu tayari wanalo na wapo tayari kulipia ili kulitatua.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,