Tunaishi kwenye zama za taarifa, zama ambazo taarifa ndiyo nguzo kuu ya mafanikio. Wale wenye taarifa sahihi ndiyo wanaoweza kufanya maamuzi sahihi na kufanikiwa sana.
Lakini pia zama hizi zimekuwa na changamoto zake, zimekuwa zama ambazo tunaweza kusema ni zama za kelele. Kwa sababu kila mtu ana nafasi ya kutoa kile anachotaka kutoa, na hapo ndipo kelele zinapoanzia.
Sasa watu wameshajifunza kwamba kila mtu anaweza kusema au kuandika, na hivyo ili kusikika wanahitaji kupiga kelele zaidi. Kusema au kuandika mambo ambayo yatawafanya watu wasikie, wakati mwingine wanakwenda kinyume na misimamo yao, ili tu wasikike. Wengine wanasema kutafuta ‘kiki’.
Dawa ya kelele hizi siyo kupiga kelele zaidi, bali kuwasiliana. Njia pekee ya kusikika kwenye zama hizi, ni kuwasiliana badala ya kupiga kelele.
Ukipiga kelele watu wameshajifunza kuzipuuza kelele, maana kelele zote ni sawa, hazina tofauti kubwa.
Lakini unapowasiliana, kuna watu watachagua kukusikiliza. Kwa sababu mawasiliano ni tofauti. Mawasiliano unakuwa na ujumbe, kwa ajili ya watu fulani na unatumia njia ambayo utaweza kuwafikia watu hao.
Lakini kelele hazina ujumbe na wala hazina watu zinawalenga, kelele zinatolewa tu, kama kuna yeyote atasikia sawa, kama wasiposikia pia sawa. Kelele ni sawa na kamari, kwamba inaweza kutokea bahati mtu akakusikia, lakini hata akikusikia anaweza asikuelewe vizuri.
Achana na kelele na anza kuwasiliana sasa. Una ujumbe ambao unataka uwafikie watu, kwanza jua ni watu gani unaowalenga, kisha jua ni kwa jinsi gani ujumbe huo unawasaidia, jua njia ipi sahihi kwako kutumia kuwafikishia ujumbe huo. Baada ya kujua hayo, toa ujumbe wako na omba mrejesho au majibu. Hapo mawasiliano yako yanakamilika, unatoa ujumbe ambao utawafikia wachache, lakini utakuwa na manufaa.
Acha wengine wapige kelele, wewe wasiliana. Achana na tamaa ya kutaka kila mtu akusikie, chagua wachache ambao unawalenga na hao watakuwezesha kuwafikia wengi zaidi.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Nikweli kocha cha msingi ni mawasiliano kwasababu kelele watu wameshajuwa namna ya kuzipuuza,uwe na siku njema.
LikeLike
Karibu sana.
LikeLike