Hakuna mwajiri mbovu kabisa amewahi kutokea hapa duniani kama mwajiri aliyekuajiri wewe. Huyu ni yule mwajiri wa kwanza kabisa, ambaye ndiye mtu wa kwanza kabisa mwenye jukumu kuu la maisha yako. Na mwajiri huyu wa kwanza kwenye maisha yako ni wewe mwenyewe.
Kama ambavyo nimewahi kukuambia, haijalishi nani amekuajiri au kukupa kazi, chochote unachofanya kwenye maisha yako, kwanza unafanya kwa ajili yako binafsi.
Haijalishi nani anaweka sahihi kwenye fedha unayolipwa, wewe ndiye mtu wa kwanza kujipa sahihi ya ulipwe zaidi au usilipwe zaidi. Wewe ndiye mwajiri wa kwanza kwenye maisha yako, iwe umeajiriwa au la.
Lakini sasa umechagua kuwa mwajiri mbovu kuwahi kutokea kwenye maisha yako.
Hebu fikiria tu wewe mwenyewe, kwa jinsi unavyofanya kazi zako, kama ndiyo kila mtu angekuwa anafanya hivyo, na wote wanakufanyia wewe kazi, unafikiri mngeweza kupiga hatua yoyote?
Kwa namna unavyoahirisha kazi zako, kwa jinsi unavyoruhusu usumbufu uingilie kazi zako, je ingekuwa una watu kumi wanaokufanyia kazi na wakafanya kama unavyofanya wewe, ungeweza kupiga hatua?
Pia jiulize upande wa kujiendeleza kwenye kile unachofanya, ni lini mara ya mwisho kujifunza kuhusiana na kile unachofanya. Lini mara ya mwisho kwako kusoma kitabu kinachohusiana na unachofanya, kuhudhuria semina, kuhudhuria mafunzo mbalimbali na hata kujiunga na kozi mbalimbali zinazohusiana na unachofanya?
Sasa fikiria wewe ndiyo umekuwa mwajiri na wafanyakazi wako wote hawajiendelezi kama ambavyo wewe hujiendelezi, unafikiri ungeweza kupiga hatua yoyote?
Rafiki, haya ninayokushirikisha hapa, ndiyo sababu kubwa kwa nini watu wengi wanaotoka kwenye ajira na kwenda kujiajiri wanashindwa. Kwa sababu unapojiajiri, unakuwa na bosi mmoja tu, ambaye ni wewe mwenyewe. Sasa tatizo la bosi huyu, ni rahisi kudanganyika kuliko bosi wa kwenye kazi za wengine.
Unapokuwa umeajiriwa, kuna kiwango cha kudanganya ambacho huwezi kukifikia. Ukichelewa kazini siku moja unaweza kutoa sababu yoyote na ukasikilizwa. Lakini unapochelewa kila siku, sababu yoyote utakayoendelea kutoa haitakupa nafasi ya kuonekana kwamba ni sahihi kwako kuchelewa.
Lakini unapokuwa umejiajiri, unaweza kuchelewa kwenye eneo lako la kazi na asiwepo wa kukuhoji kwa nini kila siku unachelewa. Utakachokuja kustuka ni pale unakuwa umeshindwa na hujui sababu ni nini. Kwa sababu hutaweza kuona kwa haraka madhara ya kuchelewa kila siku.
Hebu anza kuwa mwajiri bora kabisa kwako, anza kujiendesha kwa misingi ya ubora na siyo kuenda tu kama unavyojisikia. Angalia namna makampuni na taasisi zilizofanikiwa zinavyochukulia waajiriwa wao na wewe jichukulie hivyo. Weka njia za kupima ufanisi wako wa kazi, njia za kuendelea kujifunza kuhusiana na kazi yako na njia za kupima mafanikio yako na kujihoji pale unaposhindwa kufikia ulichopanga kufikia.
Ukianza kujisimamia wewe mwenyewe kama mwajiri mwenye msimamo mkali, utaweza kufanikiwa sana, bila ya kujali nini unafanya na maisha yako. Kuwa mwajiri bora kwako wewe mwenyewe na maisha yako yatakuwa bora sana.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,