Mpendwa rafiki,
Wazazi wengi wa siku hizi ni wazembe katika malezi, watoto wanapata sana shida wengine wanazaliwa na kuja kuteseka badala ya kufurahia kuwa duniani. Hakuna mtu ambaye amekuja duniani kwa lengo la kuteseka, wewe kama ni mzazi umepewa jukumu la kuwalinda watoto wako, kama vile mchungaji anavyolinda kondoo wake basi na wewe unatakiwa uwe hivyo.
Muda mwingine tunashindwa hata na wanyama wanavyojitoa upendo wa usadaka kwa watoto wao. Kwa mfano, sungura akitaka kuzaa lazima ajitoe yeye manyoa yake kwa ajili ya watoto wake wapate joto ni bora yeye apate baridi lakini mtoto awe salama lakini kwa wazazi wa siku hizi ni wao kwanza na watoto baadaye.
Kuna watoto wanapata changamoto nyingi kwa sababu ya uzembe wa wazazi na wengine wanafikiri jukumu la malezi ni la watu wengine, hapana ukishakuwa na mtoto jukumu la malezi ni lako yaani baba na mama na siyo la msaidizi wa kazi, wengine kila kitu wamemwchia msaidizi wa kazi hata kujua maendeleo ya mtoto wake ni shida, dunia imewakamata watu kuliko hata mambo muhimu, ni rahisi mzazi kupata muda wa kuingia kwenye mitandao ya kijamii lakini atakwambia hana muda wa kukaa na mtoto wake.

Malezi ya watoto yanataka moyo. Kuna mwanamke mmoja alikuwa na mtoto wake baada ya huyo mtoto kula maandazi kumi mtoto alidai mama naomba niongeze la kumi na moja. Mama yake mwanzoni alikataa katakata. Lakini baada ya mtoto kumsihi sana mama yake mama alikubali. Mtoto alipomaliza kula andazi la kumi na moja alimwambia hivi mama yake; mama huna hata ujasiri wa kuniambia hapana! Kweli kusema hapana yataka moyo katika malezi ya watoto.
SOMA; Watoto Wakikosa Kitu Hiki Lazima Watapotea
Dunia ya sasa unatakiwa kumfundisha mtoto kusema hapana, siyo kila kitu anachotaka basi unampatia neno hapana ni gumu na linahitaji mzazi jasiri ambaye haendeshwi na hisia kabisa, kwa sababu linaumiza lakini lina msaada sana. wengi maisha yao yanakuwa ya kizembe kwa sababu ya kushindwa kusema hapana. Tunatakiwa kuwa na kiasi, ukitumia neno hapana katika malezi ya watoto itakusaidia sana kumjengea mtoto kuwa na nidhamu ya hali ya juu.
Sina wasiwasi na mtu mwenye nidhamu kwani mtu mwenye nidhamu ni lazima kufanikiwa kwa sababu kama watu wanashindwa kujiambia hapana wao wenyewe je watawezaje kuwaambie wengine neno HAPANA. Kusema hapana inahitaji ujasiri, siyo kila kitu unatakiwa kumkubalia mtoto, unatakiwa kumwambia hapana ili ajifunze maisha.
Maisha yanahitaji nidhamu na ukizoa ndiyo kwa mtoto na kumpa kila anachotoka dunia itakuja kumwadhibu vikali pale anapokosa, ukishindwa kumfundisha mtoto wako nidhamu dunia itamfundisha kikatili sana na kumbuka huna mkataba wa milele wa kuishi na mtoto wako hivyo mpatie msingi kama vile unakufa kesho.
Hatua ya kuchukua leo; mfundishe mtoto kusema neno HAPANA,hapana itamjengea nidhamu.
SOMA; Usipomwadhibu Mtoto Wako Dunia Itakusaidia Kumwabibu Kikatili
Kwahiyo, maisha ni yoyote yanahitaji ujasiri kwa sababu kuishi tu ni ujasiri hivyo kuwa jasiri katika malezi ya mtoto kwa kusema neno hapana kwake ili ajifunze na siyo kukubali kila kitu anachotaka.
Rafiki na mwalimu wako,
Deogratius Kessy
0717101505/0767101504
deokessy.dk@gmail.com , kessydeo@mtaalamu.net
Unaweza kutembelea tovuti yangu kwa kujifunza zaidi kila siku na kupata huduma mbalimbali kama vile vitabu, kwa kutembelea tovuti hii hapa www.mtaalamu.net/kessydeo .
Asante sana na karibu sana !