AMKA Mwanamafanikio,
AMKA Kwenye siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
AMKA Na uende kwenye mapambano mapya ya siku hii ya leo.
Leo ni nafasi nyingine nzuri na ya kipekee sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.

Kwa msingi wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa TATUA, AMUA NA ONGOZA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.

Asubuhi ya leo tutafakari UIMARA WAKO AU UDHAIFU WA WENGINE?
Kigezo unachotumia kupima mafanikio yako, kina mchango sana kwenye kiwango cha mafanikio unachofikia kwenye maisha yako.

Kama unayapima mafanikio yako kulingana na uwezo uliopo ndani yako, na kule unakotaka kufika, utaweza kupata mafanikio makubwa sana na kila siku kutakuwa na hatua mpya ya kupiga.

Kama unayapima mafanikio yako kulingana na mafanikio ya wengine, unaweza kujiona umefanikiwa sana, lakini ukadumaa hapo, kama wale unaojipima nao wana mafanikio ya chini yako. Au unaweza kukata tamaa na kujiona huwezi kama wale unaojilinganisha nao wana mafanikio ya juu yako sana.

Asubuhi hii jiulize je mafanikio unayoyapigania na hata kuyafurahia ni matokeo ya uimara wako au udhaifu wa wengine?
Kama ni uimara wako uko pazuri na endelea kuweka juhudi.
Kama unajipima kwa udhaifu wa wengine, na kujiona wewe ni afadhali, unajidanganya na hutaweza kufanikiwa kwa kiasi kikubwa.

Dunia haijawahi kupata mtu wa aina yako, mtu mwenye uwezo kama wako, vipaji kama vyako na ujuzi na uzoefu kama ulionao.
Pia kwenye hii dunia hakuna mtu mwenye ndoto na maono kama uliyonayo wewe.
Hivyo kazana kifanyia kazi na kufikia uwezo mkubwa uliopo ndani yako,
Na wakati huo huo waache wengine nao wakwzane kufikia uwezo ulio ndani yao.

Mafanikio ya kweli kwako ni jinsi unavyoweza kutumia uwezo mkubwa uliopo ndani yako na siyo kuwashinda wengine.

Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kuweka juhudi ili kufikia uwezo mkubwa uliopo ndani yako na kuacha kujilinganisha na wengine.
#Fanya #HakunaSababu #NiLeoTu #IngiaMzimaMzima #AnzaNaHatuaMoja #MafanikioNiHakiYako #NidhamuMsingi #WhatEverItTakes #WachaManenoWekaKazi #SkinInTheGame #OwnTheDayOwnYourLife #UsileteSababuLetaMatokeo #MudaNiSasa

Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kocha