Rafiki,

Kama wote tunakubaliana kwamba maisha ni mchezo, basi kuna kitu muhimu sana tunachopaswa kujikumbusha kila mara kwenye huu mchezo.

Kitu hicho ni jinsi ya kushinda kwenye huu mchezo, kwa sababu bila ya kujua njia sahihi za kushinda, utakuwa umeshindwa kabla hata hujaanza.

Kwa mfano kama utaishi maisha yako kwa kujilinganisha na wengine, kama utafanya vitu ili na wewe uonekane upo au unaweza, tayari umeshashindwa kabla hata hujaanza.

Kwa sababu haijalishi utawashinda watu wengi kiasi gani, ndani yako yupo mshindani mkuu ambaye hawezi kuridhishwa na ushindi wowote wa nje. Mshindani huyu mkuu ni wewe mwenyewe na ule uwezo mkubwa uliopo ndani yako, ambao hutaweza kuutumia kama nguvu zako zote zitaelekea kuwashinda wengine.

Mchezo wowote wa kushindana na wengine kwenye maisha, kwenye kazi na hata kwenye biashara, ni mchezo ambao unakuwa umeshashindwa hata kabla hujaingia. Kwa sababu unaposhindana, unaacha kuangalia ndani yako na kuanza kuangalia wengine wanafanya nini.

Hivyo kama wale unaowaangalia wanafanya chini ya kiwango, chini ya uwezo wako, na wewe ukaonekana unafanya kuliko wao, utaridhika na kujiona umeweza sana. Lakini ndani yako bado ungeweza kufanya zaidi ya hapo ulipofika sasa, ila huwezi kwa sababu huoni kilichopo ndani yako.

Kwa mfano wewe ni kocha wa timu ya mpira wa miguu, umeenda kwenye mashindano, unaingia uwanjani na wachezaji wako 11, timu nyingine inaingiza wachezaji 20 uwanjani, je utaendelea kucheza? Vipi kama timu unayoshindana nayo itaingiza wachezaji watano tu? Hakika hutakubaliana na hali hiyo.

Sasa je kwa nini ukubaliane na hali kama hiyo kwenye maisha yako na shughuli zako?

Kama mchezo umewekwa kwa namna ambayo wewe utashindwa hata kabla hujaanza, suluhisho ni kutokucheza mchezo huo, kuangalia mchezo mwingine unaoweza kucheza, ule ambao unaendana na sheria zako wewe mwenyewe.

Kama unajiambia huwezi kufanya makubwa bila ya kuwaangalia wengine, kama unaamini ushindani ndiyo unaokusukuma, nina wazo zuri la wewe kujisukuma zaidi, kile ulichopanga na unachofanya sasa, kizidishe mara kumi, na hilo ndiyo lengo lako jipya. Kisha kuwa na mtu anayekusimamia kwenye lengo hilo jipya, ambaye hatakuacha utoroke kabisa.

Kwa njia hiyo ya kuzidisha mara kumi, utajisukuma zaidi na utaweza kuutumia uwezo mkubwa uliopo ndani yako, kuliko kuingia kwenye michezo ambayo hata ukishinda, bado unakuwa umeshinda kwa kujilinganisha na kilichopo ndani yako.

Ishi maisha yenye maana kwako, maisha yanayotumia uwezo mkubwa uliopo ndani yako.

Fanya kazi yenye maana kwako, kazi ambayo upo tayari kuifanya kwa utofauti mkubwa sana kwa kutumia uwezo mkubwa uliopo ndani yako.

Fanya biashara yenye maana kwako, biashara inayotumia uwezo mkubwa uliopo ndani yako kuwasaidia wengine na kuongeza thamani ndani yao.

Yaendee maisha yako kwa njia hii, njia ya kuchagua mchezo wako na kuweka sheria zako mwenyewe, kulingana na uwezo mkubwa uliopo ndani yako na siyo kushindana na wengine. Na kwa namna hii, mafanikio yatakuwa sehemu ya maisha yako, bila ya kujali kipi hasa umepata au kukosa.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha