Tunaishi kwenye dunia ambayo kila mtu anakazana kukimbia changamoto, kila mtu anakimbilia njia isiyo na changamoto kubwa. Kila mtu anaangalia njia rahisi ya kupata kile ambacho anataka kupata.

Na hili limezalisha kizazi ambacho kimekuwa laini laini, watu ambao hawawezi kukabiliana na changamoto kubwa, wanaosumbuliwa na msongo wa mawazo na walio rahisi kukata tamaa pale mambo yanapokuwa magumu.

Pia kwa kukimbilia njia rahisi, wengi wanakutana na kundi kubwa la watu wanaokimbilia huko, ushindani unakuwa mkubwa na manufaa yanakuwa madogo sana. Hii inapelekea wengi wawe kawaida na kushindwa kupiga hatua kubwa kwenye maisha yao.

Ninachokuambia leo rafiki yangu ni hiki, mara zote kimbilia changamoto zaidi.

Kama una njia mbili, njia moja ni rahisi na njia nyingine ni ngumu na ina changamoto, na malipo ni sawa kwa njia zote, chagua ile njia yenye ugumu na changamoto.

Kwa kuchagua ile njia yenye changamoto, utalazimika kukua zaidi, kuwa bora zaidi na kupiga hatua zaidi. Na hata kama utashindwa kwenye changamoto hizo, hutaondoka ukiwa mtupu, utaondoka ukiwa umekua zaidi ya ulivyokuwa awali.

Utakapochagua njia yenye ugumu na changamoto, utakutana na wachache sana waliochagua njia hiyo, hivyo utakuwa na ushindani mdogo na fursa za ukuaji zinakuwa kubwa zaidi. Hili pia linakupa wewe nafasi ya kukua zaidi kuliko ungechagua njia ambayo ni rahisi.

Ni sheria ya asili kwamba kitu kinakuwa imara kupitia changamoto inachokutana nayo. Chukulia mfano wa mti unaoota eneo lenye upepo na unaoota eneo lisilo na upepo. Mti unaoota kwenye upepo unakuwa imara, mizizi inaenda chini zaidi na hauwezi kuharibiwa haraka na upepo. Lakini mtu unaoota eneo lisilo na upepo unakuwa dhaifu na siku ukitokea upepo mkali unaharibika kabisa.

Chochote unachofanya kwenye maisha yako, kuanzia maisha yenyewe, kazi na hata biashara, chagua njia yenye changamoto na magumu. Najua wengi watakushangaa na unaweza kujiona kama unapotea, lakini siku nyingi zijazo, wewe mwenyewe na watu wataona jinsi ambavyo ulifanya maamuzi sahihi ya kuchagua njia hiyo.

Ukichagua njia iliyo rahisi, utapata matokeo ya haraka, lakini baadaye itakuwa ni mateso. Ukichagua njia ambayo ni ngumu, utakuwa na mateso mwanzoni, lakini baadaye ni matokeo mazuri na mafanikio makubwa. Ni wewe uchague sasa, unataka kula kwanza halafu baadaye ulipe kwa mateso, au unataka kulipa kwanza kwa mateso na baadaye ule kwa furaha.

Chagua njia yenye ugumu na changamoto, hiyo ndiyo njia yenye ukuaji na mafanikio zaidi.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha