Pamoja na siri zote za mafanikio kuwa wazi,

Pamoja na shuhuda zote za watu waliofanikiwa kuwa zinapatikana wazi kwa kila mtu.

Pamoja na misingi yote ya mafanikio kujulikana na kila mtu,

Bado mgawanyiko wa mafanikio kwenye maisha umebaki kuwa ule uke.

Kwenye kila jamii, asilimia 10 ya watu ndiyo wanakuwa na mafanikio makubwa, na asilimia 90 wanahangaika tu wasipate kile wanachotaka.

Je ni nini kinasababisha hili?

Wengi wamekuwa wanafikiria mengi, wengine mpaka wakafikia maamuzi kwamba, kuna watu wamezaliwa kutokufanikiwa. Yaani watu wamefika mahali na kukubali kwamba kuna watu wamezaliwa ili wafanikiwe, na wengine wamezaliwa kuwa tu kawaida, wasifanikiwe.

Lakini hilo sikubaliani nalo hata kidogo, uwezo wa mafanikio upo ndani ya kila mmoja wetu.

Kinachosababisha wachache sana ndiyo wafanikiwe, na wengi wasifanikiwe, licha ya wote kujua kila wanachopaswa kujua kuhusu mafanikio utayari wa kusimama mtu mwenyewe.

Sikiliza rafiki, moja ya udhaifu wetu sisi binadamu, ambao umejengwa ndani yetu kwa mamilioni ya miaka, ni kutegemea jamii inayotuzunguka kwa kila kitu. Ni vigumu kwetu kufanya kitu ambacho wengine hawafanyi. Hivyo tumekua tunaitumia jamii kama kipimo cha sisi kufanya kile tunachotaka kufanya.

Na hili lilikuwa na manufaa sana miaka elfu 5 iliyopita, kwa sababu kipindi hicho, ingekuwa hatari sana kwako kwenda msituni kuwinda peke yako. Kwa sababu hatari ya kukutana na wanyama wakali ilikuwa kubwa, hivyo kuwa peke yako ni kujipeleka kwenye kifo.

Kadhalika kwenye vyakula, kwa kuwa miaka mingi iliyopita, hatukuwa na njia ya kuhifadhi vyakula kwa muda mrefu, au kuwa na uwezo wa kupata chakula kwa wakati tunaokihitaji, tulitegemea sana jamii kwenye upatikanaji wa chakula. Hivyo kama wewe ni mwindaji, na siku moja umewinda swala, huwezi kumtunza kwa muda mrefu, hivyo unamgawa swala huyo kwa wale wanaokuzunguka. Ili kesho, ukiwa wewe hujawinda na mwenzako amewinda, basi anakupa kitoweo.

Lakini sasa hivi tunaishi kwenye zama ambazo ni tofauti kabisa, zama ambazo hatari imepungua sana, na tunaweza kusimama wenyewe kwenye mambo mengi muhimu kwenye maisha yetu. Lakini bado tunaanguka kwenye udhaifu wetu, wa kufanya yale ambayo kila mtu anafanya.

Hii ina maana kwamba, hatua ya kwanza kabisa ya kupiga ili kuweza kufanikiwa, ni kujivua kabisa gamba hili la kuitegemea jamii kwenye kila tunachofanya. Lazima mtu uwe tayari kusimama peke yako, lazima uwe na ujasiri wa kuweza kusimamia kile unachotaka, hata pale jamii na dunia nzima itakapokuwa kinyume na wewe.

Kwa sababu kila ambaye ameweza kufanya makubwa kwenye maisha yake, hakueleweka mwanzoni. Wengi waliwachukulia watu hawa kama wamechanganyikiwa, kama hawajui wanachotaka na kama watu wanaokwenda kushindwa. Lakini watu hao hawakuiangalia jamii, bali waliangalia ndani yao, na pamoja na kushindwa, mwishowe waliibuka na ushindi mkubwa sana.

Rafiki, kitu pekee unachopaswa kukitegemea kwenye mafanikio yako ni mipango yako na ukweli ambao utaupata kwa kujifunza. Lakini maoni ya wengine, ni sumu kubwa sana kwa mafanikio yako.

Kama unategemea maoni ya wengine ndiyo ufanye kitu, kama unategemea wengine wakusifie na kukubali kwa kile unachofanya, jua umeshashindwa kabla hata hujaanza. Kwa sababu utalazimika kufanya kile ambacho kila mtu anakielewa, na ukishafanya kinachoeleweka na kila mtu, unaishia kuwa kawaida.

Maoni ya wengine ni maoni, hayana ukweli sana kuhusu wewe. Ukweli pekee ulionao kuhusu wewe ni wewe mwenyewe, wewe ndiye unayejua nini hasa unataka na maisha yako, na unayejua uwezo mkubwa uliopo ndani yako, tumia nafasi hiyo kuweza kufanya makubwa zaidi kwenye maisha yako.

Hakuna kitu kikubwa utakachojaribu kufanya kwenye maisha yako halafu ukakosa watu wa kukushauri na kukukosoa kadiri ya uelewa wao, ambao hata hautokani na uzoefu. Hakuna kitu utafanya na watu wote wakakubaliana na wewe.

Hivyo usipoteze muda wako kuangalia nani anakubali na nani anapinga, jifunze ili ujue ukweli na pia angalia ndani yako ili kujua uimara wako uko wapi, kisha ongozwa na ukweli na mipango yako, na siyo maoni ya wengine.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha