“I’m here to build something for the long term. Anything else is a distraction,” Facebook cofounder Mark Zuckerberg said when he declined Yahoo’s $1 billion offer to buy his social networking service in 2006.

Hongera sana mwanamafanikio kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni nafasi bora na ya kipekee kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Kwa msingi wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa TATUA, AMUA NA ONGOZA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.

Asubuhi ya leo tutafakari KAMA HAIENDANI NA NDOTO ZAKO, NI USUMBUFU…
Hatua ya kwanza muhimu sana kwenye maisha ni kujua nini hasa unachotaka.
Hatua ya pili ni kujua gharama unazopaswa kulipa ili kupata unachotaka.
Hatua ya tatu ni kuweka kazi kulipa gharama hizo.
Mengine yote nje ya hapo ni usumbufu, yanakupotezea muda na hayakufikishi unakotaka kufika.

Kila kitu unachofanya na muda wako, kila unayekutana naye na kila mawazo unayokuwa nayo, swali la kwanza kujiuliza ni je inahusianaje na kile unachotaka? Inakuwezeshaje kufikia kitu hicho.
Kama haina uhusiano, unapoteza muda wako.

Vitu muhimu kwako ni vile vyenye mchango wa kukufikisha kule unakotaka kufika, vingine vyote ni usumbufu.
Tunaishi kwenye dunia yenye usumbufu wa kila aina, na usumbufu ni rahisi kuufikia kuliko kazi.
Lazima uwe mkali sana na muda wako, nguvu zako na umakini wako. Maana hivi ndiyo vitu vitatu watu wanakuibia kila wakati.

Fursa mpya na nzuri pia ni usumbufu.
Ukishajua nini hasa unachotaka na maisha yako, fursa yoyote unayokutana nayo, ambayo haiendani na unachotaka, ni usumbufu kwako. Ni lazima uwe tayari kusema hapana kwa vitu vizuri ili uwe na nafasi ya kupata vitu vilivyo bora zaidi.

Usiruhusu usumbufu unaokutana nao uwe kikwazo kwako kupata kile unachokutana nacho.
Usione aibu kwenye kukataa usumbufu, hata kama unatoka kwa mtu gani, kama kitu siyo muhimu, hakipaswi kuingilia kile ambacho ni muhimu zaidi.
Usikatishe kufanya kazi yako muhimu kwa sababu unaingia kwenye mitandao ya kijamii, au unafuatilia habari, au kufuatilia maisha ya wengine.

Kadiri unavyoweza kukaa mbali na usumbufu, kadiri unavyoweza kusema hapana, ndivyo unavyopata muda zaidi wa kufanya yale ambayo ni muhimu.
Kila mmoja wetu ana muda wa kutosha, kama utaacha kupoteza muda ambao tayari kila mtu anapoteza.

Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kulinda sana muda wako na kuepuka usumbufu.
#Fanya #HakunaSababu #NiLeoTu #IngiaMzimaMzima #AnzaNaHatuaMoja #MafanikioNiHakiYako #NidhamuMsingi #WhatEverItTakes #WachaManenoWekaKazi #SkinInTheGame #OwnTheDayOwnYourLife #UsileteSababuLetaMatokeo #MudaNiSasa

Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kocha