Watu wengi huwa wanaogopa kusema wamefanikiwa, kwa sababu wanajiona hawajafikia zile ngazi ambazo watu wanaoitwa wamefanikiwa wamezifikia. Hivyo mafanikio yamegeuka kuwa mbio zisizokuwa na mwisho, kama mbwa kukimbiza mkia wake, anazunguka na kuukimbiza kwa kasi lakini haukamati, kwa sababu kadiri anavyoongeza kasi, ndivyo mkia nao unaongeza kasi.

Kama hutakuwa na kipimo sahihi cha mafanikio kwako, hutajua kama umefanikiwa na utaendesha maisha yako yote ukitamani kufanikiwa bila ya mafanikio yoyote.

Hivyo hatua ya kwanza na muhimu sana kwako ni kuweka vigezo vya mafanikio yako binafsi. Achana na yale ambayo dunia inatukuza, achana na zile orodha ambazo watu wanazitumia kupima mafanikio. Kaa chini na tafakari mafanikio kwako ni nini. Na fanya hivyo kwa kuangalia maeneo yote muhimu ya maisha yako, kuanzia wewe binafsi, afya yako, kazi au biashara, fedha na hata mahusiano na wengine.

Pata picha ya maisha yako yakiwa bora kabisa kila eneo yanakuwaje, kisha chukua hatua kuiishi picha hiyo. Kwa kufanya hivi, utakuwa na maisha yenye maana kwako na pia utakuwa na sababu ya kuumia katika kufikia picha hiyo.

Baada ya kuwa na picha ya maisha ya mafanikio kwako, kutokana na vigezo vyako na jinsi unavyotaka maisha yako yawe, kuna mambo muhimu ya kuzingatia;

Moja; uhuru wa kifedha ni muhimu, hivyo lazima uweke juhudi kuufikia. Na usikazane kufikia uhuru wa kifedha ili kuwazidi wengine, bali kuweza kuwa huru kuyaendesha maisha yako namna unavyotaka.

Pili; kuna watu watakuchukia kwa sababu tu umechagua kuishi maisha yako, wapuuze watu wa aina hiyo. Usijaribu hata kidogo kuwabadili au kuwashawishi wafikirie tofauti, hutafanikiwa kwa hatua yoyote unayochukua kwa watu hao.

Tatu; wapo watu ambao watakupenda kwa wewe kuishi maisha yako, wapende na ambatana nao hao.

Nne; endelea kuwa mjinga na endelea kujifunza kila siku na kila wakati. Siku utakayojiambia unajua kila kitu ndiyo siku utakayoanza kuanguka.

Tano; kuwa king’ang’anizi, umeshaamua maisha yako yaweje, usikubali kingine bali maisha hayo, utashindwa na kukutana na vikwazo, utatamani kuachana na ndoto yako na kurudi kwenye maisha ya kawaida, hapo ndipo unapaswa kung’ang’ana zaidi.

Sita; penda sana kile unachofanya, penda sana aina ya maisha uliyochagua, penda sana kiasi kwamba huna muda wa kufikiria au kufanya ambacho hakiendani na ulichochagua.

Saba; kuwa mbunifu kila siku, usifanye chochote kwa mazoea na jaribu mambo mapya kila siku, zipe fikra zako kazi kila siku.

Nane; kopa ujuzi kwenye maeneo yako mengine, kama umewahi kufanikiwa kitu fulani, chukua somo la namna ulivyofanikiwa kwenye kitu hicho na litumie kufanikiwa kwenye kitu kingine unachofanya.

Rafiki, kwa kuchagua maana mpya ya mafanikio kwako, utakuwa na maisha ya mafanikio bila ya kujali wengine wanafikiria au wanasema nini. Na kila siku kwako itakuwa siku ya mafanikio, kama unaimaliza siku hiyo ukiwa na hekima kuliko ulivyoianza. Yote haya ni mambo ambayo yapo ndani ya uwezo wako, hayategemei uwe na akili sana, elimu sana au fedha sana ili kuyafanya. Mambo haya yanataka maamuzi na kuchukua hatua. Amua leo na chukua hatua mara moja ya kuishi maisha ya mafanikio.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha