Kanuni kuu ya uchumi, ambayo imetokana na kanuni za asili inasimamia kwenye upatikanaji na uhitaji.

Pale uhitaji unapokuwa mkubwa kuliko upatikanaji, thamani ya kitu inakuwa kubwa zaidi. Lakini upatikanaji unapokuwa mkubwa kuliko uhitaji, thamani ya kitu inashuka.

Dhahabu, shaba na chuma, yote ni madini, lakini yana thamani tofauti kutokana na urahisi wa kupatikana kwake. Ni rahisi sana kupata chuma, tembea tu mtaani utakutana na vyuma vingi vimetupwa, hivyo bei yake siyo ghali sana. Kubata shaba ni ngumu kidogo, ndiyo maana hukutani na shaba kirahisi rahisi. Lakini kupata dhahabu, ni ngumu, ngumu sana na ndiyo maana bei yake ni ya juu sana.

Hivi ndivyo soko la chochote unachofanya linapima thamani. Iwe umeajiriwa, umejiajiri au unafanya biashara, kadiri ile unachofanya kinavyoweza kupatikana kirahisi, ndivyo thamani yake inakuwa ndogo na ndivyo kipato chako kinakuwa kidogo pia. Lakini pale unapofanya kitu ambacho siyo rahisi kupatikana, thamani yake inakuwa juu na malipo yanakuwa makubwa pia.

Sasa, najua unajua hili, lakini kuna mahali umekwama. Mahali ulipokwama ni kufikiri kwamba wewe huna cha tofauti cha kufanya, hivyo umeendelea kuendesha maisha yako kwa mazoea, kufanya kile ambacho umeshazoea kufanya bila ya kuboresha kwa namna yoyote ile.

Lakini ninachokuambia ni kitu kimoja, haijalishi unafanya nini, una njia nyingi na bora sana za kufanya kwa upekee, kuwa adimu na kupandisha thamani yako zaidi.

Na sehemu ya kwanza ambayo nakushauri uanzie ni kuwa wewe. Unapochagua kuwa wewe, unapoweka utu wako kwenye kile unachofanya, unapofanya chochote kwa moyo mmoja, kama vile maisha yako yanategemea kwenye kitu hicho pekee, unatoa thamani ambayo hakuna mwingine anayeweza kutoa. Kwa sababu kama unakumbuka vizuri, hapa duniani hakuna mwingine wa kufanana na wewe.

Pandisha thamani ya chochote unachofanya kwa kuweka utu wako, kwa kuweka alama yako na kwa kufanya kwa namna ambayo hakuna anayeweza kufanya. Na hili lisikutishe kwamba unahitaji fedha sana au akili sana au watu wengi, unahitaji kuanzia sehemu moja rahisi sana, kujali zaidi.

Unapojali, unafanya zaidi na unafanya kwa utofauti, na hayo yanakuwezesha kupata matokeo bora na yenye thamani kubwa zaidi.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha