Hili siyo swali la kifalsafa wala kiimani, bali ni swali la kawaida kabisa ambalo nataka kila mmoja wetu ajiulize; wewe ni nani?

Nataka tujiulize swali hili kwa sababu zama tunazoishi sasa zimekuwa zama za kuiga kila kitu mpaka tumefikia hatua ya kujisahau sisi wenyewe, kusahau utu halisia uliopo ndani yetu.

Fikiria unavaa nguo kwa sababu umeona wengine wamevaa, unakula vyakula ambavyo wengine wanakula, unafanya kazi au biashara fulani kwa sababu ndiyo inayofanyika na wengi au kukubalika na wengi.

Tumeenda mbali zaidi mpaka kwenye imani, tunashikilia imani fulani kwa sababu ndiyo wengi wanaishikilia. Tumekosa kabisa msimamo wetu ninafsi kiasi kwamba yale unayofanya yakiwekwa kwenye mtu wa mfano, utashindwa hata kumtambua. Hii ni kwa sababu hakuna kitu hata kimoja cha uhalisia ambacho unafanya kwenye maisha yako, vitu vyote unaiga kwa wengine.

Maisha haya ya kuiga ni hatari sana kwa sababu hata kama utapata kila unachotaka, bado ndani yako patakuwa na utupu, kwa sababu utajua ya kwamba huyaishi maisha ya uhalisia kwako.

Mafanikio ya kweli siyo tu yale ya kupata mali na vingine unavyotaka, bali yale ambayo yanaleta ukamilifu ndani yako. Na ukamilifu wa ndani ni matokeo ya wewe kuishi maisha ya uhalisia wako, kufanya kile unachojali hasa na kuchagua kuishi maisha yenye maana kwako.

Kuna kiwango cha kuiga ambacho siyo kibaya, kwa sababu kupitia kuiga unajifunza kuwa bora zaidi, lakini usiige kila kitu kutoka kwa wengine, hakikisha uhalisia wako unapata nafasi ya kujionesha na fanya yale ambayo ni muhimu zaidi kwako hata kama hakuna mwingine anayefanya.

Kila wakati jiulize wewe ni nani na angalia kama maisha yako yanaakisi ule uhalisia wako. Ni njia bora ya kuepuka kujisahau na kujipoteza kwa kuiga maisha ya wengine.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha