“Don’t think about making art, just get it done. Let everyone else decide if it’s good or bad, whether they love it or hate it. While they are deciding, make even more art.” – Andy Warhol
Hongera sana mwanamafanikio kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni nafasi bora na ya kipekee sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Kwa msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa TATUA, AMUA NA ONGOZA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari FANYA KAZI YAKO…
Rafiki, kitu pekee unachopaswa kusumbuka nacho, ni kuifanya kazi yako.
Siyo kufikiria kuhusu kuifanya,
Siyo kujiandaa kuifanya,
Siyo kufikiria wengine wanaichukuliaje,
Bali kuifanya kazi.
Waachie wengine hayo ya kusumbuka na kazi hiyo,
Lakini wewe peleka nguvu na akili yako kwenye kuifanya kazi yako.
Waachie wengine jukumu la kuamua kama ni nzuri au mbaya, kama wanaipenda au hawaipendi, jukumu lako wewe ni kuifanya kazi yako.
Na wakati wengine wanaamua kazi yako iweje, wakati wanafikiria kama waipende au wasiipende, wewe endelea kufanya kazi zaidi.
Kila wakati kazana kuifanya kazi yako kwa ubora zaidi.
Na kadiri unavyoifanya kazi yako zaidi na zaidi, ndivyo unavyozalisha matokeo bora zaidi.
Itafika wakati watu watakuwa hawana namna bali kuikubali kazi yako na wewe mwenyewe.
Lakini hilo halitatokea kwa maneno, bali kwa kuifanya kazi yako.
Kile ulichochagua kufanya, kifanye kwa moyo wako wote, weka juhudi zako zote na usipoteze hata dakika moja kwenye kitu kisichohusiana na kuifanya kazi yako.
Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kuifanya kazi yako na kuwaachia wengine kufikiria na kuhukumu kazi hiyo.
#IfanyeKazi #MatendoYanaongeaKulikoManeno, #WaachieWengineKusema
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kocha